Meneja wa Mradi wa ENRICH, Bi Mwivano Malimbwi (aliyesimama) akitoa mafunzo maalum ya malengo ya mradi huo ya utoaji wa elimu ya lishe na kuboresha afya ya uzazi kwa vijana balehe kwenye  mikoa ya Singida na Shinyanga kwa waandishi wa habari ya Mkoa wa Singida (hawapo pichani)
leo, aliyekaa  ni mtaalam wa Jinsia na Utetezi wa Mradi Huo Tumaini
Fred


Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi akiangalia mazao ya asali na mashine ya kukamulia asali  ya kikundi cha ufugaji wa nyuki mkoani Singida kinachofadhiliwa wa World Vision hivi karibuni

Na. John Mapepele,Singida

Shirika la World Vision nchini  limewataka waandishi wa habari kama wadau wakuu wa Shirika  hilo  kutoa taarifa sahihi za kazi za  shirika hilo  kwenye mradi wake wa ENRICH  ambao unatekelezwa  katika  mikoa ya Singida na Shinyanga.

Mradi huo unalengo la kupeleka elimu ya lishe na afya ya uzazi kwa vijana balehe vijijini ili kupunguza  vifo vya akinamama wajawazito na watoto chini  ya siku 1000 na  ili kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano ili kuboresha maisha ya watanzania.

Akitoa mafunzo maalum  kuhusu malengo wa mradi kwa waandishi wa Mkoa wa Singida , Meneja wa Mradi wa ENRICH  Bi, Mwivano Malimbwi amesema mradi huu  ni  wa miaka mitano  kuanzia mwaka 2016 hadi mwaka  2021 na umejikita katika  kuwezesha  huduma za lishe ili kuimarisha afya  ya  mama na mtoto  kwa gharama za dola  milioni 8.4 za kikanada.

 Kwa mujibu wa Malimbwi  malengo  mahususi ya ENRICH ni kupunguza  vifo vya akina mama na watoto  kwa kuangalia  visababishi  vya vifo hivyo ambapo mradi umeelekeza nguvu kwenye kuimarisha mifumo ya utoaji wa afya katika vituo vya kutolea  huduma  hizo.

Aliongeza kuwa awali wakati mradi ulipoanza  walibaini  changamoto ya upatikanaji wa vifaa vya kumchunguza hali ya kiliishe ya mtoto  vilikuwa na upungufu mkubwa ambapo  vituo vichache  vilikuwa na  vifaa hivyo vya kupimia urefu na mzingo wa kati wa mkono kwa akina mama na mtoto

Alisema kuwa watoa huduma wachache walipata mafunzo ya afya ya lishe  kwenye ngazi ya mkoa na wilaya ambapo  hakukuwa na watoa huduma katika maeneo ya vijijini.

Aidha alisema pia hakukuwa na elimu ya uongozi kwenye kamati za afya za mikoa  na wilaya ambapo Mradi uliwajengea uwezo ili kuwa sehemu ya  kuleta mabadiliko kwa pamoja  badala ya kuwa watoa maamuzi. 

Aidha mipango na bajeti ilikuwa ikifanywa kwa hisia  badala ya kutumia takwimu sahihi.

Malimbi amesema lengo la  pili  la Mradi ni kuongeza uzalishaji wa chakula  chenye uwingi wa virutubisho ambapa kwenye eneo hili amessisitiza kuwa mkakati umekuwa  katika kuongeza  uzalishaji ulioongezwa kibailojia, kuongeza utumiaji wa virutubishi kwa watoto na sayansi ya ulaji na ufyonzaji wa virutubishi,

Alisema pia katika mikoa ya Singida na Shinyanga imebarikiwa kuwa na  vyakula vya makundi yote na matunda ya asili kama sasati, rade na furu ambayo kama yakitumika kikamilifu yatasaidia sana kuboresha lishe na kupunguza udumavu kwa watoto.

Alipongeza jitihada za Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Dk. Rehema Nchimbi  kuwa  mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa suala la lishe na afya ya uzazi vinakuwa kipaombele cha kwanza kwa wananchi ambapo pia amesema amehamasisha ulaji na ulimaji wa viazi lishe na kuwafanya wananchi wa Mkoa wa Singida tofauti na awali ambapo vilikuwa vikiuzwa nje ya Mkoa.

Aidha amesema Mradi umehamasisha akina mama kulima bustani za mbogamboga kwenye kila kaya ili kuhakikisha kuwa  kwenye kila mlo mboga zinakuwepo.

Amesema lengo la mwisho la mradi  huo  ni kuhakikisha  kuwa  kunakuwa na uwajibikaji wa wadau wote muhimu na kila mmoja anafanya majukumu yake kwa ufasaha, ambapo ametolea mfano kuwa Serikali kama mdau mkuu ina wajibu wa kuweka  vituo vya kutolea huduma na mtoa huduma ambapo jamii inawajibu wa kuvitumia vituo hivyo na watoa  huduma.

Mradi wa ENRICH ni Mradi wenye sekta nyingi na unafadhiliwa na Serikali ya  nchi ya Canada ambapo unatekelezwa kwa kushirikiana  na wabia ambao ni Nutritional International, Canadian Society for  International Health anayejikita katika kuimarisha mfumo wa afya.

Ikiwemo Harvest Plus, kwenye Sekta ya Kilimo, Chuo kikuu cha Toronto  katika kufanya tathimini na ufuatiliaji wa mradi na World Vision ambaye ni msimamizi mkuu wa fedha wa mradi huo. Serikali ya Tanzania ni mtekelezaji namba moja chini ya TAMISEMI.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: