Wadau wa madini nchini   wameipongeza Tume ya Madini kwa elimu bora kuhusu shughuli za utafiti, uchimbaji na biashara ya madini  na kuongeza kuwa elimu hiyo itawasaidia sana kuboresha ushiriki wao kwenye Sekta ya Madini.

Wadau hao wametoa pongezi hizo leo tarehe 19 Septemba, 2020 katika Maonesho ya Tatu Ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini  yanayoendelea katika Uwanja wa Kituo cha Uwekezaji cha Bombambili Mkoani Geita.

Wakizungumza katika nyakati tofauti wadau hao wamesema kuwa walikuwa na uelewa mdogo juu ya namna ya kuomba na kupata leseni za madini pamoja na namna bora  ya uendeshaji wa shughuli za uchimbaji na biashara ya madini lakini kupitia maonesho husika wamepata elimu ya  namna kupata leseni,namna bora ya uendeshaji wa shughuli za uchimbaji na biashara ya madini.

Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji wasio rasmi wanaoendesha shughuli zao katika eneo la Mwakitolyo Mkoani Shinyanga Mohamed Ramadhan alisema kuwa mara baada ya kupata elimu husika, wataunda kikundi na kuomba leseni ili waanze kuchimba na kupata faida huku wakilipa kodi mbalimbali Serikalini.

Naye Lazaro Paul ambaye ni mchimbaji mdogo anayechimba madini ya dhahabu katika eneo la Kakola mkoani Shinyanga alisema kuwa, kabla ya kupewa elimu na wataalam wa Tume ya Madini alikuwa hafahamu taratibu za uchimbaji wa madini na kuongeza kuwa kuanzia sasa ataomba leseni na kuanza kuchimba madini rasmi.

“Baada ya kupata elimu safi kutoka kwa wataalam nitaomba leseni ya kuchimba madini ya dhahabu mkoani Morogoro maana ninatambua kuwa sasa ninaweza kumiliki leseni ya madini kwa kufuata taratibu,” alisema Paul.

Aidha, Edward Makanza ambaye ni mchimbaji mdogo katika Mgodi wa Buckreef uliopo  mkoani Geita aliongeza kuwa kupitia maonesho hayo amepata uelewa wa namna ya kuendesha shughuli za uchimbaji wa madini kwa kuzingatia usalama wa mazingira.

Naye Mhandisi Uchenjuaji wa Madini kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), Cosmas Festo aliipongeza Tume ya Madini kwa elimu inayotolewa mara kwa mara kwa wadau wa madini nchini.

Akielezea lengo la ushiriki wa Tume ya Madini kwenye maonesho hayo, Mtakwimu wa Tume ya Madini, Azihar Kashakara alisema kuwa ni pamoja na kuelimisha wadau wa madini hususan wachimbaji wadogo kuhusu namna ya kuomba leseni za madini, namna bora ya uendeshaji wa shughuli za uchimbaji na biashara ya madini.

Alisema kuwa kumekuwepo na changamoto ya wananchi wengi kutokuwa na uelewa wa namna ya kuomba leseni za madini, uchimbaji salama na biashara ya madini.

Aliongeza kuwa sambamba na elimu inayotolewa kupitiwa maonesho na mikutano mbalimbali, Tume ya Madini imekuwa ikiwakutanisha wachimbaji wa madini na Taasisi za Kifedha kama vile benki za CRDB na NMB ili kuwapa uelewa wa pamoja kuhusu uendeshaji wa shughuli za uchimbaji na biashara ya madini ili waweze kupewa mikopo na benki husika.

Aliendelea kusema kuwa pia Tume ya Madini imeendelea kutenga maeneo yaliyofanyiwa tafiti kwa ajili ya kugawa kwa wachimbaji wadogo wa madini.

Naye Mhandisi Migodi wa Tume ya Madini, Edward Mumba alieleza kuwa kupitia Kurugenzi ya Ukaguzi Migodi, Mazingira na Baruti wamekuwa wakitoa elimu mbalimbali kwenye maeneo yenye shughuli za madini zinazoendeshwa na wachimbaji wadogo ili kuhakikisha wanazalisha kwa faida kwa kuzingatia usalama wa afya na mazingira.








Share To:

msumbanews

Post A Comment: