Na John Walter- Manyara

Mgombea Mwenza wa Kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amesema chama Cha mapinduzi kwa uongozi makini waliouonyesha kuwaongoza wananchi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kinastahili kuendelea kuongoza.

Samia  ameyasema hayo wakati akizindua awamu ya Pili ya Kampeni za Ccm kitaifa septemba 27,2020 katika wilaya ya Kiteto Mkoa wa Manyara.

Samia  amesema kwenye Miundo Mbinu Mkoa wa Manyara  katika ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi mwaka 2020-2025, wamepanga  Kukamilisha na Kuanza upembuzi yakinifu na usanifu wa kina Katika barabara za Kongwa Ranch - Kiteto - Simanjiro - KIA (km 483);  Babati -Orkesumet - Kibaya (km 225);  Mbulu - Magugu (Mbuyu wa Mjerumani) (km 63;) Babati (Dareda) – Dongobesh (km 60).

Aidha katika ilani ya Chama cha Mapinduzi kuhusu Wafanyabiashara Wadogo, imeeleza kuwa yametengwa maeneo rasmi  kwa ajili ya wajasiriamali wakiwemo mama lishe na wauza mbogamboga kufanyia biashara katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Manyara.

Kuhusu Kilimo Samia  amesema Chama cha Mapinduzi kimefanikiwa kufanya Ukarabati na ujenzi wa  bwawa la Dongobesh (Halmashauri  ya Wilaya ya Mbulu) ambao umekamilika.

Akizungumzia Nishati, amesema ilani  hiyo ambayo awamu inayomalizika imefanya mengi itaendelea kuhakikisha wananchi wote wanapatiwa umeme kwenye nyumba zao  bila kujali aina  ya nyumba wanayoishi.

Amesema serikali ya Ccm imetekeleza Mpango Kabambe wa Kupeleka Umeme Vijijini (REA I, REA II na REA III) ambapo jumla ya vijiji 8,587 kati ya vijiji 12,319 vya Tanzania Bara vimefikiwa na umeme ambayo ni sawa na asilimia 70; pamoja na Kupunguza gharama za kuunganisha umeme vijijini ambapo gharama za kuunganisha umeme vijijini zimepungua kutoka wastani wa shilingi 454,000 hadi shilingi 27,000; huku  kasi ya usambazaji wa umeme vijijini ikiongezeka.

Akizungumza kuhusu Afya Mgombea Mwenza huyo  wa Urais amesema CCM inatambua kuwa huduma za afya ni muhimu katika kuhakikisha
wananchi wanakuwa na afya bora ili kuwawezesha kushiriki katika
shughuli za maendeleo ya nchi ambapo katika Mkoa wa Manyara ukarabati unefanyika  katika vyumba vya upasuaji, wodi za kulaza wagonjwa, jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na wodi za wazazi na watoto na kuwekewa vifaa vya kisasa vya upasuaji na maabara.

Kwa upande wake Mgombea Ubunge Jimbo la Kiteto Edward Ole Lekaita amewaomba wananchi wa Kiteto wampe kura za ndio yeye, Madiwani wa ccm  pamoja na Rais ili kuwawakilisha bungeni.

Samia  Suluhu Hassan ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yupo katika ziara  mkoani Manyara kwa ajili ya Kampeni kunadi Sera za Chama cha Mapinduzi na Wagombea nafasi za Udiwani, Ubunge na Rais kupitia Chama hicho.

Share To:

Post A Comment: