NA ANDREW CHALE, CHALINZE.

MGOMBEA Ubunge wa Chama Cha Mapinduzi CCM anayewania kiti hicho kwa mara nyingine, Mhe. Ridhiwani Kikwete amezindua rasmi kampeni zake za Ubunge Jimbo la Chalinze huku akiwataka WanaCCM kupiga kura za kishindo kwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Ridhiwani Kikwete amesema kwa sasa WanaCCM watembee kifua mbele kwani maendeleo yameoenekana kutokana na utekelezaji wa Ilani ya CCM ikiwemo ile ya 2020-2025.

"Tumeshuhudia miundombinu bora na ya kisasa pamoja na ukuaji wa huduma za kijamii ikiwemo afya, pia elimu na maendeleo ya utawala bora.

Oktoba 28, WanaCCM Chalinze, Bagamoyo na Tanzania kwa ujumla tujitokeze kifua mbele kumpigia kura nyingi za ndiyo Rais Magufuli lakini pia kura za ushindi kwa Madiwani  na Wabunge wetu." alisema Ridhiwani Kikwete.

Aidha, akinadi sera na maendeleo yaliyopatikana  ndani ya jimbo hilo, 
Alisema awali wakati anaingia kwenye jimbo hilo alikuta vituo vya afya vitano lakini kwa sasa vimeongezeka na kufikia zaidi ya Nane.

"Leo hii tulipo kuna vituo vya Afya zaidi ya Nane na kuwa vikisaidia sana Wananchi wetu kupata huduma stahiki mahala pao na kuacha kwenda mbali.

Lakini pia kwa sasa tunaendelea kupanua katika ujenzi wa vituo vyetu vya afya ikiwemo kituo cha Afya Buringu, pia tunataka kujenga wodi ya akinamama kama kituo cha Miono,

Hii itaenda kituo cha afya Kibindu na vingine ilikuhakikisha Wananchi wetu hawaendi mbali kusaka huduma za afya." Alisema Ridhiwani Kikwete.

Aidha, aliongeza kuwa lengo kubwa yeye kama Mbunge na Madiwani watahakikisha Wananchi wa Chalinze wanapata huduma za afya zikiwemo za kibingwa ndani ya Chalinze.

"Miaka mitano iliyopita tumehakikisha Wananchi wanapata huduma za afya hapahapa. Katika kuhakikisha hilo tayari Hospitali imeshajengwa na ipo katika hatua ya mwanzo.

Ujenzi wake upo wa vipande vya hatua nne kwa sasa tunaingia hatua ya pili ambapo wodi ya kutoa huduma kwa akina mama nayo imeanza kujengwa

lengo mimi kama mbunge na Madiwani ni kuhakikisha hospitali ile inajengwa na kukamilishwa kwa ukamilifu ili Wananchi wetu wasiende tena Hospitali za Wilaya za jirani kama Tumbi ama Bagamoyo ili waweze kufaidika na matunda ya viongozi wao" Alieleza Ridhiwani Kikwete.

Akiongelea suala la miundombinu, tayari maji, umeme na barabara kwa kuzingatia ilani, imetekelezwa kwa kiwango kikubwa na kwa sasa amewataka wananchi wajiandae kwa mambo makubwa.

"Ilani ya CCM 2020-2025  Imeelezea juu ya utekelezaji sasa wa ujenzi wa barabara ya Afrika Mashariki inayotoka Kenya inayopita Pangani inayokuja mpaka Saadani na kwenda Mkange hadi Makurunge na Bagamoyo.

Wananchi wa Mkange mliopitiwa na barabara hii mtalipwa fidia na mjiandae sasa kwa mambo makubwa yanayokuja kwani mji unakuja kubadilishwa

Pia maisha ya watu yatabadilika na uchumi utakuwa mkubwa sana na zao la muhogo unaolimwa utakuwa na thamani kubwa sana" Alisema Ridhiwani Kikwete.

Aidha, Ridhiwani Kikwete aliwataka wote waliopita bila kupingwa kuhakikisha wanaendelea kumuombea kura nyingi za chama cha Mapinduzi CCM Rais Magufuli wakiwemo Wabunge wa vitimaalum ili kushinda ushindi wa kishindo.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni hizo, Katibu Mkuu Mstaafu, Kinana alisema misingi imara iliyojengwa na viongozi wa chama hicho itaendelea kulindwa na kuimalisha ushindi imara.

"Wote ambao mliteuliwa Chama kwenye majimbo na vitimaalum hongereni sana.
Pia hongereni kwa mliopita bila kupingwa, lakini msibweteke, mpambane kutafuta kura nyingi za Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli." alieleza Kinana.

Kinana pia aliweza kuwaombea kura madiwani wote wa Jimbo la Chalinze na Bagamoyo pamoja na Mgombea wa Ubunge wa Bagamoyo,  Muharami Mkenge.

Uzinduzi huo umefanyika katika  viwanja vya Miono shule ambapo umati mkubwa wa wananchi na wanachama wa CCM waliweza kushiriki kusikia sera mbalimbali za wagombea wao.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: