Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akifungua  maonesho  ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi mmoja Jijini Dar es Salaam
Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Charles Kihampa akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonesho ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia.
Baadhi ya viongozi mbalimbali wa Taasisi za Elimu walioshiriki katika maonesho ya 15 ya elimu ya Juu Sayansi na Teknolojia wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo.


Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo ametoa wito kwa Vyuo Vikuu nchini kuhakikisha vinaanzisha programu za masomo zinazoendana na vipaumbele vya kitaifa.

Dkt. Akwilapo ametoa wito huo Jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa maonesho ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia ambapo amesema kwa kuanzisha programu hizo nchi itaongeza ujuzi wa wataalamu na pato la taifa.

Kiongozi huyo ametaja baadhi ya programu za kipaumbele kuwa ni mafuta na gesi, afya, hususani udaktari bingwa kwa ngazi za Uzamivu katika nyanja zote za magonjwa ya upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu, upandikizaji figo, ini na uboho (bone marrow), tiba za ndani za moyo, na uhudumiaji wa wagonjwa wa dharura na mahututi (emergency medicine and critical care).

 “Tusingependa kama nchi kupeleka wagonjwa wetu nchi za nje kutibiwa, bali nchi za nje waje kutafuta tiba kwetu (medical tourism). Kwa kufanya hivyo tutaongeza ujuzi wa wataalamu wetu pamoja na pato la taifa,” amesisitiza Dkt. Akwilapo.

Katibu Mkuu Akwilapo ameongeza kuwa pamoja na kuanzisha programu za vipaumbele, nchi kwa sasa inatekeleza miradi mingi mikubwa ambayo inahitaji wasomi wa kuendesha na kusimamia miradi hiyo, hivyo ni jukumu la Taasisi za Elimu ya Juu kuhakikisha hili linafanyika kwa ufanisi wa hali ya juu kwa kuhakikisha wanatoa elimu bora na kwamba Serikali itaendelea kusomesha kwa wingi wataalamu katika fani na ujuzi adimu na maalum kwa mahitaji ya nchi.

“Ni jambo la kutia moyo kuona kwamba hivi sasa baadhi ya vyuo vikuu vimeanza kuelekeza jitihada zao katika kutoa elimu ambayo inalenga kushughulikia changamoto za jamii na kuweka msisitizo katika maeneo ya kimkakati ya nchi kama vile Kilimo, Madini, Utalii, Uvuvi, Maliasili na Misitu na Afya,” amesema Dkt. Akwilapo. 

Katika hatua nyingine Dkt. Akwilapo ameendelea kuzitaka Taasisi za Elimu ya Juu kuona namna bora ya kupanua udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu kutokana na ongezeko la udahili wa wanafunzi katika ngazi ya msingi na sekondari na kwamba wanapohitimu lazima wapate nafasi katika vyuo vya kati na vya juu ili kuweza kuwapa ujuzi wa kujiajiri na hivyo kuchangia kikamilifu katika ujenzi wa Taifa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Vyuo Vikuu nchini, Profesa Mayunga Nkunya  amesema Tume pamoja na mambo mengine imefanikiwa kuimarisha mfumo wa utoaji ithibati ya mtaala, jambo ambalo lilionekana kuwa tatizo kwa muda mrefu na kwamba itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kuwatumikia Watanzania katika sekta ya elimu ili kuhakikisha Watanzania wa ngazi zote wanapata elimu bora yenye kukidhi viwango vya ubora Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.

Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini, Profesa Charles Kihampa amesema lengo la maonesho hayo ni kutoa fursa kwa vyuo vikuu kujitangaza na kuonesha huduma na kazi wanazofanya pamoja na mchango wao katika ustawi wa elimu ya juu kwa mustakabali wa maendeleo ya sayansi, teknolojia na manuufaa yake kiuchumi na kijamii.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi waliotembelea maonesho hayo wamesema wamefurahishwa na kuwepo kwa maonesho hayo kwani yanatoa fursa ya kuonana na wahusika na kupata taarifa zinazowawezesha kuomba programu zinazoendana na ufaulu wao.

Jumla ya taasisi 67 za elimu ya juu zimeshiriki katika maonesho hayo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: