Na Immaculate Makilika na Jonas Kamaleki – MAELEZO
Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato ya Kodi, Maduhuli, Tozo na Huduma Mbalimbali za Serikali (GePG) unatajwa kusaidia kuokoa fedha nyingi za Serikali zilizokuwa zikipotea kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo udanganyifu.
 
Akizungumza jana jijini Dodoma wakati akipokea  Ripoti ya Tathimini ya Mfumo wa Kielektroniki ya Ukusanyaji wa Mapato na Usimamizi wa Fedha za Umma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James alisema kuwa mfumo wa GePG ulianzishwa Julai 2017 ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizokuwepo serikalini wakati wa ukusanyaji wa fedha za umma umesaidia Serikali kuokoa fedha nyingi zilizokuwa zikipotea kutokana na changamoto mbalimbali.
 
Katibu Mkuu huyo alitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni gharama kubwa za miamala inayohusu makusanyo ya fedha za umma, utaratibu usio rafiki kwa mlipaji wa huduma za umma, ugumu wa kupata taarifa ya makusanyo yanayofanyika kwa wakati huo huo, pamoja na machaguo machache ya njia za kulipia (Benki, Mitandao ya simu za mkononi au Mawakala) kwa sababu kuongeza machaguo kulikuwa kunaongeza gharama za ukusanyaji kwa taasisi.
 
“Mfumo wa GePG umewezesha kuongezeka kwa makusanyo ya Serikali kwa ujumla wake na kwa taasisi moja moja. Mfano makusanyo ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) yameongezeka kutoka shilingi  bilioni 95.0 kabla ya kuanza kwa mfumo hadi kufikia shilingi  bilioni 115.0 kwa mwaka baada ya kuanza kutumia mfumo wa kielektroniki”, alisema Doto.
 
Aliongeza “Wakala wa Vipimo  umeongeza mapato yao  kutoka kiasi cha shilingi bilioni 1.0 kwa mwezi kabla ya mfumo wa GePG hadi kufikia  kiasi cha shilingi bilioni 2.5 kwa mwezi baada ya kujiunga na GePG.  Pia, taasisi nyingine zimepunguza gharama walizokuwa wanalipia ada za miamala ya kielektroniki inayohusu makusanyo ya fedha za umma. Kwa mfano TANESCO ilikuwa ikilipa zaidi shilingi bilioni 38 kwa mwaka kwa mawakala wa kuuza umeme. Baada ya kufunga mfumo wa GePG kwa sasa Shirika halilipi chochote”.
 
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, William Erio alisema kuwa GePG tangu  shirika hilo lijiunge na mfumo huo mwaka 2019 umesaidia kutatua changamoto mbalimbi pamoja na kuongeza mtaji wa Shirika.
 
“GePG imeleta mabadiliko makubwa na imesaidia utendaji wa mfuko ambapo katika kipindi kifupi cha miaka miwili tu thamani ya Mfuko imeongezeka hadi kufikia asilimia 40, kutoka makusanyo ya shilingi bilioni 600 hadi kufikia shilingi trilioni 1.1 kwa mwaka”, alisema Erio.
 
Naye, Mhasibu Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Peter Mwakosya alisema kuwa licha ya mfumo wa GePG kusaidia katika ukusanyaji wa mapato kutoka katika vyanzo  mbalimbali, mfumo huo umeondoa tatizo la hundi feki, malipo hewa pamoja na kupunguza matumizi ya akaunti za ukusanyaji wa fedha kutoka 30 hadi kufikia 5 zilizokuwa zikitumiwa na TFS.
 
Katika kukabiliana na changamoto za ukusanyaji na usimamizi wa fedha za umma, Wizara ya Fedha na Mipango imebuni mifumo mikubwa minne ya kielektroniki na kutengeneza na kusimamia mifumo minne ambayo ni Mfumo wa Ukusanyaji wa Mapato ya Kodi, Maduhuli, Tozo na Huduma Mbalimbali za Serikali (GePG); Mfumo wa Usimamizi na Udhibiti wa Matumizi na Malipo ya Serikali (MUSE), Mfumo wa Usimamizi  wa Miradi ya Maendeleo (NPMIS)  na Mfumo wa Usimamizi wa Misamaha ya Kodi.
 
Wasilisho hilo lilitolewa na Dkt. Joel Mtebe wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye aliongoza timu ya Tathimini ya Mfumo wa Kielektroniki ya Ukusanyaji wa Mapato na Usimamizi wa Fedha za Umma.

Mwisho.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: