Tuesday, 15 September 2020

Bima yawataka watumishi wa serikali kukatia bima vifaa vya maofisini


Shirika la Bima la Taifa Mkoa wa Arusha limewataka wadau wa shirika hilo kuhakikisha wanakatia bima vifaa mbalimbali vya maofisini na mitambo ili kujiweka katika mazingira mazuri zaidi ya kufidiwa  pale kunapotokea majanga ya ajali.

Kauli hiyo imetolewa Jana na Meneja wa  Bima Mkoa wa Arusha na Manyara ,John Mdenye wakati akiongea na wadau wa shirika hilo kutoka taasisi mbalimbali za serikali na halmashauri kutoka mikoa hiyo,waliohudhulia semina ya mafunzo ya bima yaliyofanyika jijini Arusha.

Alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwakumbusha kwamba wao kama wadau wa bima wanawajibu wa kuunga mkono shirika hilo ambalo ni Mali ya serikali katika kukatia bima vifaa muhimu vilivyosahaulika ikiwemo mitambo.

"Tumeamua kuwakumbusha taasisi za serikali kukatia bima vifaa mbalimbali kwani wengi wamezoea kukata bima za magari pekee na kuacha vifaa vingine muhimu katika utendaji wao kazi"

Katika hatua nyingine meneja huyo alionya baadhi ya wateja wa shirika hilo wenye tabia ya udanganyifu wanaoteketeza Mali zao walizokatia bima ili walipwe ,kuwa shirika hilo lipo macho na watu wenye tabia hiyo kwani wanavyo vifaa vya hali ya juu kubaini matukio na wahusika watashughulikiwa na vyombo vya dola

Kwa upande wake Alfred Bojo ambaye ni Afisa wa shirika la bima tawi la Arusha alisema kuwa mafunzo hayo yamewashirikisha maafisa wa taasisi za serikali kwa mikoa ya manyara na Arusha kupata uelewa wa masuala ya bima.

Alisema kuwa mafunzo hayo ni pamoja na kuwapa uelewa wa kujua jinsi gani ya kufanya pale wanapopata ajali ili waweze kufidiwa kwa muda mfupi zaidi.

"Kwa sasa shirika letu linatoa fidia ndani ya siku saba pale mhusika atakapokuwa amekamilisha taratibu muhimu zinazohitajika"alisema Bojo

No comments:

Post a comment