Benki
ya Dunia imeitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 50 duniani za uchumi
wa kipato cha kati, ikiwa ni ya pili baada ya Kenya katika nchi za
Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, baada ya ukuaji wa uchumi unaosukuma
pato la mwananchi kukua (Per capita GNI) mwaka 2020.
Tanzania
imeingia kwenye uchumi wa kati miaka mitano kabla ya lengo la Dira ya
Taifa ya Maendeleo ya 2025, jambo ambalo ni la kujivunia.
Akizungumza
katika Mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dodoma, Katibu Mkuu
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa
Serikali, Dkt. Hassan Abbasi alisema kwa mujibu wa Dira ya Taifa ya
Maendeleo, 2025 katika ukurasa wa pili, kipengele 1.2 “Uchumi wa kipato
cha kati umehusishwa na kuwa na nchi ambayo umaskini unapungua, uchumi
imara unaojengwa na kuimarika kwa uzalishaji viwandani unaimarika na
wananchi wanapata maendeleo”.
Dkt.
Abbasi alisisitiza kuwa uchumi wa kipato cha kati umegawanyika katika
madaraja mawili daraja la chini ambapo ni kuanzia dola za Kimarekani
1036 hadi 4045 na daraja la juu ni dola 4046 hadi 12,535 na mwaka huu
Tanzania imepanda daraja kuwa uchumi wa kipato cha kati daraja la chini,
pamoja na nchi za Algeria na Benin.
Aidha,
Dkt. Abbasi alifafanua siri 10 zilizoisaidia Tanzania kutajwa kufikia
daraja la uchumi wa kipato cha kati na Benki ya Dunia hapo Julai 1,
2020 kuwa ni nchi yenye amani na utulivu, na hivyo ni msingi muhimu
nyuma ya mafanikio ya nchi ya Tanzania kuingia katika uchumi wa kipato
cha kati kwani bila amani hakuna kufanyakazi, hakuna kuzalisha na
hakuna kuongeza kipato. Na hivyo viongozi, wanahabari na wananchi kwa
ujumla wamesisitizwa kuwekeza akili zao katika kuimarisha amani
iliyopo na kukataa chokochoko zozote zile zinazoweza kuharibu misingi ya
maendeleo.
Siri
ya pili ni mipango thabiti ya maendeleo, ambapo Dkt. Abbasi alisema
kuwa moja ya kanuni muhimu ya kuendelea ni kuwa na mipango inayokuwekea
malengo makubwa (Olympic targets). Serikali itaendelea kuweka mipango
mbalimbali ya maendeleo ya muda mrefu na mfupi, akitolea mfano mwaka
2020 Serikali ilianza kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025
ambayo moja ya malengo ni kufikia uchumi wa kati.
Kwa
mujibu wa Dkt. Abbasi siri ya tatu ni utekelezaji usioyumba, katika
miaka 59 ya Uhuru na mitano ya Awamu ya Tano Serikali imejitahidi
kusimamia eneo hilo kwa kuhakikisha mipango inayowekwa inatekelezwa kwa
kina (3feet implementation).
Siri
nyingine ni maamuzi magumu, “Moja ya mafanikio ya Serikali ya Tanzania
kwa Awamu zote na sasa tumeimarisha katika Awamu ya Tano ni wakati
fulani Serikali kufanya uamuzi mgumu ambao wakati fulani ulionekana kuwa
ni ndoto lakini baadaye ukaleta mafanikio makubwa kwa jamii,
tumepambana na wala rushwa na wahujumu uchumi, tumewekeza katika
miundombinu mikubwa, tumekataa pia baadhi ya nadharia za kimagharibi
kwenye utendaji wetu na utungaji wetu wa sera za maendeleo” alisema Dkt.
Abbasi.
Aidha,
Dkt. Abbasi alitaja siri nyingine kuwa ni azma ya kujitegemea, nidhamu
katika matumizi, kutekeleza miiko ya uongozi, kuwekeza kwenye miradi
inayochechemsha uchumi, maendeleo ya vitu na sekta binafsi yenye tija.
Post A Comment: