Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeruhusu michezo ya kirafiki kuendelea  kwa masharti ya kuzingatia mwongozo uliowekwa kuhusu tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona.

Uamuzi huo umefikiwa leo June 9, baada ya kikao cha TFF na klabu za Azam, KMC, Simba, Transit Camp na Yanga ambazo katika mechi zao za kirafiki zilizochezwa hivi karibuni kutozingati masharti yaliyotolewa na Wizara ya Afya.

Katika kikao hicho, klabu hizo zilikubaliana na TFF kuwa zitafuata mwongozo wa Wizara ya Afya kama ulivyotolewa, ikiwemo kuweka majukwaani watu wao (social distancing agentes) ili kuhakikisha washabiki wanakaa kwa kuachana nafasi.

Hivyo, mechi ya kirafiki iliyopangwa kuchezwa kesho Jumatano kati ya Azam FC na KMC  katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Saa 1:00 usiku ndiyo itakayokuwa ya mfano katika utekelezaji wa makubaliano hayo.

Klabu hizo zimeomba radhi kwa hali iliyotokea katika mechi zao za kirafiki lakini vilevile maofisa habari wa vilabu hivyo watahamasisha mashabiki wao kuzingatia mwongozo wa Wizara ya Afya katika kukabiliana na virusi vya Corona kupitia vyombo vya habari.

Kwa upande wa Simba, Uwanja wao wa Mo Simba Arena uliopo Bunju, jijini Dar es Salaam hautatumika tena kwa ajili ya mechi za kirafiki kwa vile uwanja huo ni maalumu kwa mazoezi tu.
Share To:

Post A Comment: