Kamanda Polisi wa Ilala, Kamishna Msaidizi Zuberi Chembera akipokea salamu kwa ukakamavu kutoka kwa Koplo Brown Twaibu kabla hamjamkabidhi cheti cha pongezi kwa kazi nzuri aliyofanya katika kupambana na Covid-19. Koplo Twaibu alijizolea umaarufu baada ya video kusambaa akiwahimiza abiria kwenye daladala kufuata maelekezo ya serikali kama kuvaa barakoa ili kujilinda na kuwalinda na wengine.Wengine katika picha Mkuu wa Mawasiliano wa Benki ya NBC, David Raymond. na Meneja wa Tawi,NBC Mnazi Mmoja Sada Matitu.



BENKI ya Kibiashara ya  NBC imetambua juhudi mahususi za Jeshi la Polisi Tanzania na maofisa wake katika  kipindi chote cha mlipuko wa homa kali inayosababishwa na virusi vya Covid-19 maarufu kama corona. 

Katika matukio mbali mbali ya kipekee, maofisa kwa Jeshi la Polisi Tanzania wameonyesha  hekima ya hali ya juu na dhamira ya kuwatumikia, kuwalinda na kuhakikisha Watanzania  wanatekeleza maelekezo ya wataalam ya jinsi ya kupambana na ugonjwa wa corona. 

Aidha, benki hiyo ikishirikiana na Jeshi la Polisi Tanzania pia imemtambua na kumpongeza Koplo Brown Twaibu Msoke kwa kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuvaa barakoa katika kupambana 
na gonjwa la corona.

 Koplo Twaibu alijizolea umaarufu baada ya video ikimuonyesha akiwahimiza abiria kwenye daladala kufuata maelekezo ya serikali kama kuvaa barakoa, kutosimamisha abiria  kwenye usafiri wa umma na kukaa umbali wa mita moja siyo kwa kujilinda tu bali kuwalinda na 
wengine. 

Akiongea katika hafla hiyo, Mkuu wa Mawasiliano wa NBC David Raymond amesema  “Kufikia maamuzi ya kumpongeza Koplo Twaibu ilikuwa kitu rahisi kwa benki yetu, hususani kwa  sababu vitendo vyake vya kishujaa vinaendana na msimamo wa benki yetu katika kupambana na virusi vya Covid-19.” 

Amesema, Itambulike kuwa Benki ya NBC pia imechukua hatua madhubuti kupamba na kuenea kwa virusi hivyo kama kuwa benki ya kwanza kuweka vitakasa mikono katika ATM zake zote nchini, utekelezaji wa nafasi ya mita mbili katika matawi yake. 

Raymond amesema benki yao pia itaendelea  kuwahamasisha na kuwaelimisha wafanyakazi wake na Watanzania kwa ujumla jinsi ya  kumpambana kwa ugonjwa huo. 

Aidha RPC Ilala Zuberi Chembera amesema, “Koplo Twaibu ameonyesha mfano mzuri wa  kuhamasisha jamii juu ya uvaaji wa barakoa kwa dhumuni la wananchi kujikinga na kuwakinga wengine dhidi ya maambukizi ya virusi vya korona. Kitendo hicho ni mfano wa kuiga na kinahitaji  pongezi ya pekee hususan kipindi hiki ambacho dunia nzima inapambana na janga hili. 

Pamoja Benki ya NBC kumtunuku Koplo Brown Msoke fedha taslim TSHs. 1,000,000 na kumfungulia  akaunti katika benki hiyo, Jeshi la Polisi Tanzania pia limemzawadia Koplo Twaibu kiasi cha TSHs  200,000 na cheti maalumu kutoka kwa Kamanda wa Polizi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa.


Katika kuendeleza dhamira ya kuelimisha jamii matumizi sahihi ya barakoa, Benki ya NBC  imezindua kampeni yake mpya ya #NBCBarakoaChallenge. Pamoja kuhimiza uvaaji wa barakoa,  kampeni ya #NBCBarakoaChallenge itakayoendeshwa kupitia mitandao ya kijamii ya NBC  inaangalia pia kuwakumbusha na kuelimisha Watananzania juu ya umuhimu wa kuzingatia tabia  kinga ili kuzuia Covid-19. 
Share To:

Post A Comment: