Na John Walter-Manyara
Hakimu mfawidhi wa wilaya ya Hanang’ mheshimiwa Aman Shao amemhukumu kwenda jela miezi kumi na mbili au kulipa faini ya shilingi elfu hamsini kwa kila kosa kwa makosa saba, aliyekuwa mratibu wa chanjo wilaya ya Hanang Mkojera Philemon.
Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Manyara Holle Makungu amesema hukumu hiyo imetolewa Mei 29,2020.
 Amesema kuwa waendesha mashtaka wa TAKUKURU Isdory Kyando na Evalyne Onditi walimfikisha mahakamani hapo Philemon na kumfungulia Kesi ya Jinai Namba CC 89/2018 akishtakiwa kwa makosa saba ya ubadhirifu wa fedha za chanjo ya Surua aliyoyafanya mwaka 2014 kinyume na sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa Namba 11/2007.
Katika mashtaka hayo saba,mshtakiwa aliorodhesha majina ya watumishi wa Halmashgauri ya wilaya ya Hanang’ kuonyesha kuwa aliwalipa fedha kwa ajili ya safari ya chanjo ya surua na Rubela huku akijua sio kweli na akajipatia fedha kwa njia ya ubadhirifu huo shilingi milioni  nne laki nne na elfu ishirini na tano (4,425,000/=).
Amesema baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na pande zote mbili,mheshimiwa Shao aliridhika kwamba mshtakiwa alitenda makosa hayo na hivyo kumpa adhabu ya kwenda jela miezi kumi na mbili kwa kila kosa au kulipa faini hiyo ya shilingi laki tatu na nusu (350,000) na hivyo kukwepa kutumikia kifungo.
Makungu ameeleza kuwa Philemon amepata adhabu hiyo inayoonekana kuwa yenye unafuu kwa kuwa makosa aliyoshtakiwa nayo aliyatenda mwaka 2014 kabla ya sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007 haijafanyiwa marekebisho.
Makungu ametumia nafasi hiyo kuwafahamisha watumishi wa Umma na wananchi kwa ujumla kwamba, mwaka 2016 bunge la jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nia thabiti ya kuhakikisha rushwa inatokomezwa hapa nchini,lilipitisha sheria namba 3/2016 ambayo iliidhinishwa kwa kutiwa sahihi na Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Joseph Magufuli tarehe 7 julai 2016.
Ameongeza kuwa sheria hiyo ilianza kutumika rasmi tarehe 8 julai 2016 baada ya kutangazwa katika gazeti la serikali, na kwamba katika sheria hiyo makosa karibu yote ya sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007 yakiwemo ya ubadhirifu,matumizi mabya ya madaraka,uchepuzi pamoja na matumizi ya nyaraka kumdanganya mwajiri kama aliyofanya Philemon yamekuwa ni makosa ya uhujumu uchumi.
Amesema kwa msingi huo ni kwamba mtu ukipatikana na hatia mahakamani kwa makosa ya sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa  namba 11/2007 yaliyotendeka kuanzia tarehe 8 julai 2016,adhabu iliyoainishwa na sheria ya bunge namba 3/2016 ni kifungo kisichopungua miaka ishirini jela na kisichozidi miaka thelathini.
Amebainisha kuwa pamoja na adhabu hiyo, sheria namba 3/2016 inaelekeza pia mali zilizopatikana kutokana na makosa ya rushwa zitaifishwe na kurejeshwa serikalini na kwamba katika mabadiliko hayo hakuna mbadala wa faini.
Mkuu huyo wa TAKUKURU mkoa wa Manyara  ametoa rai kwa watumishi wa Umma kujiepusha na vitendo vya rushwa na wale wenye masikio lakini hawataki kusikia wataanza kukumbana na adhabu hiyo kali hivi karibuni.

Share To:

Post A Comment: