Na Mwandishi wetu
MKUU wa mkoa wa Tanga, Mhe. Martine Shigela amesema kampeni ya elimu kwa mlipakodi ambayo inaendeshwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itawasaidia wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi kuacha vitendo hivyo ambavyo huikosesha Serikali mapato.

Mhe. Shigela alitoa kauli hiyo ofisini kwake wakati alipotembelewa na maafisa wa TRA wanaofanya kampeni hiyo mkoani hapa ambayo imelenga kuwaelimisha wafanyabiashara kuhusu masuala ya kodi ikiwa ni pamoja na kuwakumbusha kulipa kodi kwa wakati.

Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa, kuna baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakikwepa kulipa kodi pengine kwa kujua au kutokua, jambo ambalo linahitaji elimu ya uelewa ili kila mwananchi afahamu wajibu wake kwenye ulipaji wa kodi kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Akielezea kampeni hiyo, Mhe. Shigela ameipongeza TRA kwa kuendesha zoezi hilo katika mikoa mbalimbali na kusema litaongeza ukusanyaji wa mapato baada ya wafanyabiashara kuelimishwa na kufahamu kuwa maendeleo ya nchi yanasababishwa na ulipaji wa kodi kwa ajili ya kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, barabara, umeme na maji.

Mhe. Shigela amewataka wafanyabiashara kuhakikisha wanalipa kodi kwa hiari bila kusubiri kubugudhiwa na serikali, huku akieleza kuwa serikali itaendelea kupambana na wakwepa kodi wanaoingiza bidhaa za magendo nchini kwa kupitia bandari bubu zilizopo kandokando ya Bahari ya Hindi.

“Nchi yoyote haiwezi kupiga hatua ya maendeleo bila wananchi wake kuwa na utamaduni wa kulipa kodi kwa sababu kodi ndio kila kitu huwezi kujenga barabara kama wafanyabiashara hawataki kulipa kodi, huwezi kuimarisha huduma za afya kama hakuna kodi na pia huwezi kuimarisha mifumo ya elimu bila kodi,” alisema Mhe. Shigela.

Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Mkoa wa Tanga, Bi. Specioza Owure alisema kuwa, maafisa hao wa TRA wanaofanya kampeni ya elimu kwa mlipakodi, watafika maeneo mbalimbali yenye wafanyabiashara katika mkoa wa Tanga na watawaelimisha kuhusu umuhimu wa kodi na kuwahamasisha kulipa kodi kwa wakati.

“Maafisa hawa wanatumia jitihada zote kuwaelimisha wafanyabiashara, tunafanya hivi ili kila mmoja afahamu wajibu wake wa kulipa kodi sambamba na kusogeza huduma za TRA karibu na wateja,” alisema Owure.

Kampeni ya elimu kwa mlipakodi mkoani Tanga itamalizika tarehe 30 Juni, 2020 ambapo lengo la kampeni hiyo ni kutoa elimu ya kodi kwa wafanyabiashara, kusikiliza maoni na changamoto zao ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha kulipa kodi kwa wakati.

Share To:

Post A Comment: