Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameusifu uongozi wa Wilaya ya Nkasi unaongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mh. Said Mtanda pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Missana Kwangura kwa kutekeleza maagizo ya Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mh Suleiman Jafo kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa na hatimae wananchi wameanza kupata huduma katika hospitali ya Wilaya hiyo.
Wakati akitoa pongezi hizo Mh. Wangabo alisema kuwa hivi karibuni tarehe 2.6.2020 Mh. Jafo alifanya ziara katika Wilaya ya Sumbawanga na kuzitaka hospitali mpya 67 za Wilaya nchini kuanza kufanya kazi kuanzia tarehe 8.6.2020. ili kufikia lengo lililotarajiwa la kuwasaidia wananchi kupata huduma za kiafya katika ngazi ya Wilaya.
Aidha, Mh. Wangabo alisema kuwa serikali ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli imeongeza Shilingi bilioni 1.4 kwa hospitali tatu za Wilaya ambapo kila hospitali imepatiwa shilingi milioni 300 kwaajili ya kuelekezwa kwenye maeneo ambayo yanatakiwa kukamilishwa katika ujenzi wa hospitali hizo wakati Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga imepatiwa Shilingi Milioni 500 kwaajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali mpya ya Manispaa hiyo.  
“Nilipokuwa naingia tu imenishangaza, yaani nilifikiri imeanza kutumika miezi sita iliyopita, lakini ni ndani ya wiki moja, mazingira haya yameboreshwa namna hii na kila kitu kipo kwenye mpangilio wake, tunastahili kupongezana, lakini pongezi za aina yake ziende kwa uongozi wa wilaya hii ya Nkasi, Mheshimiwa DC tumpigie makofi, amesimamia vizuri san ana anaendelea kusimamia vizuri sana, Wilaya yake, lakini Siwezi kuacha kumpongeza sana Mkurugenzi wetu wa halmashauri ya Wilaya ya Nkasi,” Alisema.
“Jambo jingine ambalo ningependa wananchi mfahamu, Mheshimiwa Dokta John Pombe Joseph Magufuli ametoa tena shilingi bilioni 1.4 katika mkoa wetu wa Rukwa, Kila hospitali ya Wilaya katika zile tatu, zitapata milioni 300 na tayari fedha hizi zipo, Rais wetu Dkt. Hohn Pombe magufuli anatupenda sana, na fedha hizi ni lazima zitumike ndani ya mwezi huu kabla ya mwaka wa fedha haujaisha, Mkurugenzi wa Nkasi hakikisha kwamba milioni 300 zinaelekezwa kwenye maeneo yale ambayo yametakiwa kuelekezwa,” Alisisitiza.
Pia aliwaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha maeneo yote ya hospitali hizo yanapimwa na kupatiwa hati haraka iwezekanavyo ili kuepusha migogoro na wananchi ambao wanazunguka maeneo hayo kwa kufanya shughuli za kilimo.
Awali akisoma taarifa ya uzinduzi wa huduma za afya katika hospitali ya Wilaya ya Nkasi Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt Hashim Mvogogo alisema kuwa huduma ambazo zimeanza kutolewa katika hospitali hiyo ni pamoja na wagonjwa wa nje (OPD), Meno (Dental Clinic), Macho (Eye Clinic), Kujifungua, Kliniki ya Wajawazito na Watoto na huduma ya Maabara.
“Jumla ya Watumishi 28 tumewabadilisha kutoka katika vituo mbalimbali na kuwaweka katika hospitali hii ambayo tunaifungua leo (8.6.2020), aidha, dawa na vifaa tiba tumefanya ‘re-allocation’ kutoka katika vituo mbalimbali ndani ya Wilaya yetu ili kuhakikisha kuwa huduma hii tunaweza kuitoa,” Alieleza.
Kwa upnde wake Mganga mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu alisema kuwa baada tu ya kupokea maagizo kutoka kwa Mh. Jafo, Katibu Tawala Mkoa aliteua wataalamu wachache kutoka ngazi ya Mkoa akiwemo Mganga Mkuu huyo kwaajili ya kuratibu utekelezaji wa maagizo hayo na kuifanya kazi hiyo kwa kushirikiana na Wakurugenzi wa halmashauri pamoja na timu za afya ngazi za wilaya.
“Na kwa watumishi ninavyowaona naona huduma hasa za OPD zimeanza kama ilivyoagizwa, tulielekezwa kuanza na huduma za awali, kwa maana ya huduma za wagonjwa wa nje lakini ikiwezekana huduma za wazazi, kama ulivyosikia kwenye taarifa, lakini baada ya muda mfupo ujao tunategemea hospitali yetu ianze kutoa huduma zote,” Alisema.
Kwa upande mwingine, Mh. Wangabo alitembelea hospitali ya Wilaya ya Kalambo ambayo hakurudhishwa na mazingira aliyoyakuta baada ya hospitali hiyo kukamilika kwa asilimia 76 huku maeneo mengi yakihitaji kumaliziwa ili huduma zianze kutolewa kwa wananchi.
Share To:

Post A Comment: