mkurugenzi wa  Star  Intalinational Iringa  Dkt  Jesca  Msambatavangu akizungumza na  wanahabari mkoani Iringa (hawapo pichani) wakati  akizindua mfumo wa  ufundishaji  wanafunzi wa  shule za  sekondari na msingi kupitia mitandao ya  kijamii (online)  wakiwa nyumbani  kwa  kujiunga  kupitia Tovuti ya www.coronaseasonschool.com 

..............................................

Na  Francis  Godwin,  Iringa 

Uongozi  wa shule ya  Star  Intalinational Iringa  umezindua mfumo   mpya  wa ufundishaji  wa  wanafunzi wa sekondari na  shule za msingi nchini kwa  njia ya mitandao ya  kijamii (Online)  ambapo  wanafunzi  watafundishwa   wakiwa  majumbani .

Akizungumza na wanahabari jana  wakati akizindua mpango  huo wa  ufundishaji  kwa  njia ya mtandao  mkurugenzi wa  Star  Intalinational Iringa  Dkt  Jesca  Msambatavangu  alisema  kuwa  mfumo  huo utamwezesha  mwanafunzi wa  sekondari na yule wa shule za msingi  kuweza  kuendelea na masomo kama  kawaida  kwa  wakati huu ambao  shule  zimefungwa .

"  Kutokana na changamoto ya  virusi vya  Corona  ambavyo  vimeikumba dunia   sisi kama   wadau wa  elimu  tumeona  kila mmoja kwa nafasi yake  anapaswa  kuangalia  namna gani ya  kuwasaidia   watoto  wa kitanzania  ambao kwa sasa  wanaendelea  kukaa nyumbani pasipo  kufundishwa " 

 Hivyo  alisema   kwa upande wa  shule yake kutokana na changamoto   hiyo  alilazimika  kubunia mbinu  hiyo ya ufundishaji  wanafunzi  wake  majumbani kwao  kwa  kuwapa kazi mbali mbali za  kufanya na kusahishiwa   kwa mtandao  bila ya  kukutana na mwalimu .

Alisema kupitia  mfumo  huo  wa  kimtandao  wameweka utaratibu wa  kila darasa   ndani ya wiki  kuweza  kukutana na mwalimu  kwa  njia ya mtandao ambapo  wanafunzi  wataweza  kufundishwa moja  kwa moja (live) na  kuweza  kuuliza maswali  mbali mbali  ya kimasomo  kutokanana  kazi  walizopewa .

Hata  hivyo  alisema   mfumo  huo wa ufundishaji  utawalenga  wanafunzi   wote  wa Tanzania wanaosoma  sekondari na  shule za msingi ambapo  ili  waweze kuendelea na masomo  yao wakiwa nyumbani watatakiwa   kujiunga na tovuti ya  www.coronaseasonschool.com ama   kupiga  simu  0716 79 79 79 au 0653 797979.

Dkt  Msambatavangu  alisema  kwa  kupitia mfumo   huo  wa kimtandao  wajibu wa mzazi  utakuwa ni  kuhakikisha  wanawasimamia   watoto  wao  kufanya kazi  ambazo  zinatolewa kupitia mtandao  na   kuzingatia  vipindi .

Kwani  alisema  badala ya  wazazi  kuwaacha  watoto  wao wakitumia muda  mwingi  kucheza ama kutazama TV  nyumbani ni vizuri  sasa  watoto hao  wakazingatia  muda wa masomo  kwa  kujiunga na mfumo  huo  rafiki  kuweza  kuendelea  na masomo  na kuwa masomo yamezingatia mitahala ya Tanzania .

Pia  alisema  anaendelea na mchakato  na  ikiwezekana  basi  mfumo   huo  kuuwezesha  zaidi ili  kufundisha masomo  ya  shule za Msingi na Sekondari  kwa  nchi  zote za Afrika  na  kuwa  wameamua  kuweka gharama ndogo  sana kwa   wazazi wa  kitanzania  kwa  ajili ya kujiunga na mfumo   huo ili  watoto  wao kujisomea  na kuwa  hata kama shule  zitafunguliwa bado mfumu  huo hautafungwa  utakuwa  endelevu 

Kwa  upande  wao  baadhi ya  wazazi  mjini  Iringa  wamepongeza  uzinduzi wa  ufundishaji  kwa  njia ya  mtandao na  kuwa utasaidia  watoto  wao kuendelea  kujisomea  wakiwa nyumbani tofauti na ilivyo kuwa  siku 30  za mwanzo baada ya  serikali  kufunga  shule na watoto  kukosa kufundishwa .

Tukuswiga  Mwaisumbe  alisema  kuwa  kupitia mfumo  huo mzazi  sasa atalazimika  kujaza kifurushi kwenye  simu janja ama  kwenye Kompyuta  ama Laptop  ili  kumwezesha   mtoto wake  kuweza  kuendelea na masomo na kuomba uongozi wa  shule  hiyo  kuja na kuhamishia mfumo  huo kwenye radio za  kijamii ili  wananchi wa  vijijini nao waweze  kuwawezesha  watoto wao kuendelea na masomo.

Huku Anani Ndelwa  alisema  kuwa  kuanzishwa kwa mfumo  wa masomo mtandaoni ni  hatua kubwa na ya kujivunia kwa Tanzania  kwani kupitia mfumo   huo watoto  wataweza  kugeuka tabia  na kuachana na matumizi ya mitandao ya kijamii  kutazama katuni ama picha   zisizo na maadili .





  

Share To:

Francis Godwin Mzee wa matukiodaima

Post A Comment: