Wadau Wamkabidhi Waziri Mkuu Sh. Bil 6.226 Kukabili CoronaWAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea kutoka kwa wadau msaada wa fedha pamoja na vifaa mbalimbali kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) wenye thamani ya sh. bilioni 6.226.

Baada ya kupokea kupokea msaada huo, Waziri Mkuu amewashukuru wadau hao kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya virusi vya corona, ambapo hadi sasa kesi 24 zimeripotiwa tangu kuanza kwa ugonjwa huo nchini na wagonjwa watano wamepona.

Waziri Mkuu amepokea msaada huo leo (Jumatano, Aprili 8, 2020) katika Ofisi Waziri Mkuu Mlimwa, jijini Dodoma. Amewataka Watanzania waendelee kushirikiana na Serikali katika kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.

Amesema hadi sasa jumla ya watu 396 wapo kwenye karatini katika maeneo mbalimbali yaliyotengwa wakiwemo wageni wanaoingia nchini ambao wanafuatiliwa afya zao na baada ya siku 14 kama watakuwa hawana maambukizi wataruhusiwa kuungana na familia zao.

Waziri Mkuu amesema Serikali kwa upande wake imeendelea kuchukua mbalimbali katika kupambana na ugonjwa wa COVID-19 na kwa sasa imejiimarisha kwenye utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kujikinga na virusi vya corona.

“Serikali inatoa misitizo kwa wananchi wazingatie maelekezo yanayotolewa kuhusu kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona ikiwemo kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka pamoja na kujiepusha na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo ili kuzuia usisambae kwa sababu hadi sasa mkoa huo unaongoza kwa kuwa na wagonjwa zaidi wa corona nchini.

Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuvishukuru vyombo vya habari nchini kwa ushirikiano wanaoutoa katika kuelimisha umma namna ya kujikinga na virusi vya corona pamoja na wasanii waliotunga nyimbo za kuuelimisha umma namna ya kujikinga na ugonjwa huo.

Miongoni mwa wadau waliotoa msaada huo ni kampuni ya Madini ya Twiga iliyotoa sh. bilioni nne, mfanyabiashara maarufu nchini Rostam Aziz ametoa sh. bilioni moja, kampuni ya Taifa Gesi imetoa sh. milioni 100 na kampuni ya mafuta ya Puma imetoa msaada wa mafuta lita 50,000 zitakazotumika katika magari yanayotoa huduma za kupambana na corona nchini yakiwemo magari ya kubebea wagonjwa.

Wengine ni kampuni ya TEHAMA ya Huawei imetoa vifaa kuendeshea mikutano kwa njia ya video ambavyo ni cloudlink camera tatu, Cloudlink Mic tatu, Cloudlink TV terminal tatu, Cloudlink Platform pamoja na Thermal Imaging Temperature Measuring System moja vyote vikiwa na thamani ya sh. milioni 940, Asasi za Kiraia (AZAKI) zimetoa sh. milioni 79.

Baada ya kupokea misaada hiyo, Waziri Mkuu kwa niaba ya Rais Dkt. Magufuli aliwashukuru wadau hao kwa vitu mbalimbali walivyovitoa kwa ajili ya kupambana na COVID-19 kwani vifaa pamoja na fedha walizozitoa zitaisadia Serikali katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Kuhusu wadau wengine wanaohitaji kutoa misaada, Waziri Mkuu amesema ofisi yake iko wazi pia wanaweza kupeleka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na kwa walio nje ya nchi au sehemu yoyote wanaweza kutuma fedha kupitia akaunti Na: 9921159801 yenye jina la National Relief Fund Electronic.

Awali, mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Azizi alisema ametoa sh. bilioni moja ambayo ameielekeza katika kununua vitakasa mikono ambavyo vitatumiwa na wasafiri wa daladala wa Dar es Salaam na Zanzibar ili waweze kutumia kabla ya kupanda usafiri huo, hivyo kuweza kujikinga.

Pia, Mfanyabiashara huyo ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa kuwaongoza Watanzania kwa hekima na busara na kuwaepusha na taharuki kama ilivyotokea katika mataifa mengine. Amempongeza Waziri Mkuu na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa namna wanavyoshiriki katika kukabiliana na corona.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Share To:

msumbanews

Post A Comment: