Wizara ya Madini imesema hakuna majadiliano yoyote
yanayoendelea kati ya Serikali na Kampuni ya TanzaniteOne na
badala yake Leseni ya Kitalu C iliyokuwa inamilikiwa na kampuni
hiyo kwa ubia na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) imefutwa
kwa mujibu wa Sheria na tayari eneo hilo limerudishwa Serikalini
na hakuna mwekezaji mpya.

Kauli kuhusu suala hilo zilitolewa Machi 11, 2020 kwa nyakati
tofauti na Waziri wa Madini, Doto Biteko, Katibu Mkuu wa Madini
Prof. Simon Msanjila na Mkurugenzi wa Leseni Tume ya Madini
Mhandisi Yahaya Samamba wakati wa kikao kazi kati ya Wizara
na Kamati ya Eneo lililodhibitiwa la Mirerani (Mirerani Controlled
Area) kilichofanyika Jijini Dodoma.

Mbali na Kamati hiyo, kikao hicho pia kilihudhuriwa na Waziri wa
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi, Naibu
Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi
Joseph Nyamhanga, Mkuu wa Wilaya ya Simajiro Mhandisi
Zephania Chaula ambaye ni Mwenyekiti wa Eneo lililodhibitiwa la
Mirerani, pamoja na Uongozi wa Tume ya Madini.

Waziri Biteko alisema hatua ya kufuta leseni hiyo ilikuja kufuatia
maelekezo yaliyotolewa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Serikali baada ya Kamati Maalum iliyoundwa
kuchunguza biashara ya Madini ya Tanzanite kubaini kuwa leseni
hiyo ilitolewa kinyume cha Sheria.

Waziri Biteko aliongeza kuwa, hivi sasa Serikali inaangalia namna
bora ya kuligawa eneo hilo kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na
taratibu ili kuhakikisha kwamba madini ya Tanzanite yanakuwa na
manufaa zaidi kwa Taifa na kuchochea ustawi na maendeleo ya
nchi kupitia madini hayo na kuongeza kuwa, serikali iliwashirikisha
wadau kupata maoni ya namna ya kuligawa eneo husika.

‘’ Serikali nzima inaangalia eneo la Mirerani, eneo hilo linahitaji
mazingira rafiki ili wachimbaji wafanye shughuli zao kwa amani na
usalama na serikali ipate mapato yanayostahili. Wajibu wetu kama

wizara ni kuhakikisha ukuta wa mirerani unapandisha mapato ya
serikali,’’ alisisitiza Waziri Biteko.
Pia, aliongeza kuwa, ndoto yake kama Waziri wa Madini ni kuona
biashara ya Tanzanite inafanyika ndani ya ukuta katika Kituo cha
Pamoja cha Biashara ya Madini ya Tanzanite (One Stop Center)
kilichojengwa na serikali na kuongeza kuwa, hata hivyo, serikali
haizuii madini hayo kuuzwa katika masoko mengine.

Vilevile, Waziri Biteko alitaka mamlaka zinazohusika na usimamizi
wa eneo hilo kuhakikisha zinatekeleza majukumu yao kwa mujibu
wa sheria na taratibu zilizowekwa bila kuvuruga taratibu na
kuongeza kuwa, ‘’ Tume ya Madini iliundwa maalum kwa ajili ya
usimamizi wa rasilimali madini’’.

Katika hatua nyingine, Waziri Biteko alizitaka Ofisi za Madini nchini
kuhakikisha zinatoa ushirikiano kwa taasisi nyingine za serikali
katika masuala yanayohusu Sekta ya madini ili kuweka mazingira
rahisi ya utekelezaji wa majukumu katika sekta, zikiwemo Kamati
za Ulinzi na Usalama katika maeneo husika.


Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
Hussein Mwinyi aliishauri wizara kutoa taarifa kwa wizara hiyo
endapo itakuwa na mahitaji maalum ya ulinzi katika eneo hilo na
kutumia fursa hiyo kukipongeza kikosi maalum kinachofanya kazi
eneo hilo kwamba, kinatekeleza wajibu wake ipasavyo.

“ Mhe. Waziri nafurahi kusikia kwamba, Jeshi Mirerani linatekeleza
majukumu yake kikamilifu na hakuna mwingiliano. Endapo
mtakuwa na mahitaji maalum mtatutaarifu sisi,’’ alisema Waziri
Mwinyi.

Naye, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akizungumza
katika kikao hicho, alizitaka taasisi za Serikali zinazozimamia sekta
ya madini kuhakikisha zinaelewa na kufahamu matakwa ya Sheria
zinazosimamia sekta ya madini.

‘’ Ni vizuri kukumbushana mara kwa mara na ni vizuri wadau
wajue kuwa kutokujua sheria siyo tiketi ya kuvunja sheria,’’
alisema Naibu Waziri.
Akitoa ufafanuzi kuhusu mpaka wa eneo la Kitalu C, Katibu Mkuu
wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila alisema kuwa mpaka

uliowekwa mwaka 1987 ndiyo halali na huo ndiyo msimamo wa
Wizara ya Madini. Akizungumzia suala la miundombinu ya
TanzaniteOne, alisema kuwa, serikali itaweka utaratibu maalum
wa namna ya kushughulikia suala hilo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Mhandisi Joseph
Nyamhanga alizitaka taasisi za umma kuhakikisha zinazingatia na
kutekeleza kwa weledi matakwa ya Sheria ya Tawala za Mikoa ili
kuwezesha utekelezaji mzuri wa majukumu ya serikali.

Awali, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Wizara ya Madini Edwin
Igenge, alitoa mada kwenye kikao hicho kuhusu Kanuni za Madini
(Udhibiti wa Eneo la Mirerani, 2019) kwa lengo la kujenga uelewa
wa pamoja katika usimamizi wa shughuli za eneo hilo.
Naye, Mkurugenzi wa Leseni Tume ya Madini Mhandisi Yahaya
Samamba alitoa mada kuhusu Historia ya Uchimbaji Madini ya
Tanzanite na Changamoto zake, ambapo alieleza kuwa, Tume ya
Madini iliifuta Leseni ya Tanzanite mnamo tarehe 23 Desemba,
2019 baada ya kampuni ya TML kuandika barua serikalini
Desemba 10 kuomba kuachia eneo hilo na mbia mwenza
STAMICO aliridhia ombi hilo Desemba 19, 2019.

Kikao hicho kilijadili masuala mbalimbali yanayohusu shughuli
za uchimbaji Madini ya Tanzanite, changamoto na namna ya
kuzitatua pamoja na usimamizi wa eneo hilo, kwa lengo la
kuboresha shughuli za uchimbaji wa Tanzanite, biashara ya
Tanzanite ikiwemo kuhakikisha Serikali inapata mapato stahiki
kupitia madini  hayo kufuatia uwekezaji mkubwa uliofanywa na
Serikali wa ujenzi wa Ukuta unaozunguka machimbo ya Tanzanite,
Mirerani.
Share To:

Post A Comment: