Friday, 13 March 2020

REDCROSS WATOA MSAADA WA VIFAA VYA KUKUSANYIA DAMU SALAMA KIGOMANa Editha Karlo, MsumbaTv Kigoma
Imeelezwa kuwa ukosefu mkubwa wa vifaa vya kufanyia kazi wakati wa zoezi la ukusanyaji damu katika wilaya mbalimbali za mkoa Kigoma umekwamisha mpango wa kukusanya damu ya kutosha kwa ajili ya benki ya damu mkoani humo.

Meneja mradi wa damu salama mkoa Kigoma, Abichi Maramba akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo kwa Mganga Mkuu wa mkoa Kigoma, Simon Chacha kwa niaba ya kituo cha damu salama mkoani humo alisema kuwa wakati mwingine uhamasishaji unafanyika lakini ukosefu wa vifaa unakwamisha zoezi hilo.

kutokana na changamoto hiyo alisema kuwa shirika  la msalaba mwekundu Tanzania mkoa Kigoma kupitia mpango wa damu salama limetoa vifaa mbalimbali kwa ajili ya kusaidia zoezi la ukusanyaji damu mkoa Kigoma ili kukabiliana na changamoto ya upungufu mkubwa wa damu salama inayokikabili kituo cha damu salama mkoani humo.

Meneja mradi wa damu salama mkoa Kigoma, Abichi Maramba akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo kwa Mganga Mkuu wa mkoa Kigoma, Simon Chacha kwa niaba ya kituo cha damu salama mkoani humo alisema kuwa vifaa vyote vilivyotolewa vina thamani ya shilingi milioni 67.

Akivitaja vifaa vilivyotolewa kuwa ni pamoja na viti vinavyotumika wakati wa zoezi la kutoa damu 16,madaa na vitendanishi vinavyotumika wakati wa zoezi hilo genereta kubwa la kufua umeme kwa ajili ya kituo cha kuhifadhia damu,friji moja ya kuhifadhia damu,  Computer seti moja,Mashine ya kupima magonjwa mbalimbali (Biochemistry machine) kwa ajili ya hospitali ya mkoa Kigoma maweni na mashine ya uchunguzi wa magonjwa (Microscope) kwa ajili ya kituo cha afya Makere wilaya Kasulu.

Awali Mratibu wa maabara na damu salama ofisi ya Mganga Mkuu wa mkoa kigoma, Stanley Ngereza alisema kuwa kutokuwepo kwa vifaa vya kufanyia kazi wakati wa kuendesha zoezi la uchangiaji damu vijiji imekuwa changamoto kubwa inayofanya zoezi hilo kutofanyika mara kwa mra licha ya uhamasishaji unaofanyika na wananchi kujitokeza.

Ngereza alisema kuwa kutolewa kwa vifaa hivyo na Shirika la Msalaba mwekundu kupitia mpango wa damu salama kutasaidia kukabiliana na changamoto hiyo na kwamba hali hiyo itaongeza chachu ya upatikanaji wa kiasi kikubwa cha damu mkoani Kigoma na kuifanya benki ya damu kuwa na damu wakati wote.

Mganga Mkuu wa mkoa kigoma,Simon Chacha akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa mkoa Kigoma alisema kuwa msaada huo wa vifaa kwao ni jambo kubwa katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya ikiwemo upatikanaji wa damu wakati wote pindi wagonjwa wanapohitaji.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment