Mkuu wa mkoa wa Iringa Ally Hapi wa pili kushoto akimtazama mwanafunzi wa shule ya sekondari Mazombe aliyeanguka kwa njaa
Wanafunzi wa sekondari ya Ibumu wakirejea nyumbani
Mkuu wa mkoa wa Iringa Ally Hapi akipongezwa na wananchi wa Ibumu
..........................
Na Francis Godwin, Iringa
BAADA ya wanafunzi watatu wa shule ya sekondari Mazombe wilaya ya Kilolo kuangua kwa tatizo la njaa wakati wakimsikiliza mkuu wa mkoa wa Iringa Ally Hapi wakati wa ziara yake ya Iringa mpya awamu ya pili ,mkuu huyo wa mkoa ameagiza wazazi wote kuchangia chakula kwa ajili ya watoto wao .
Akitoa agizo hilo mkuu huyo mkoa alisema kuwa tatizo la wanafunzi kuanguka kutokana na njaa sio zuri kwa maendeleo ya elimu katika mkoa wa Iringa ambao unaongoza kwa uzalishaji wa mazao ya chakula hivyo ni lazima wazazi wote kuhakikisha wanachangia chakula kwa ajili ya watoto wao ili kila shule uwepo mpango wa wanafunzi kupata chakula kwa pamoja.
Kwani alisema mazingira wanayotoka wanafunzi hao yametofautiana na wapo ambao wanatoka asubuhi pasipo kula chakula chochote hivyo kushinda shule bila kula ni tatizo jingine ambalo linapelekea mwanafunzi kukosa uwezo wa kumsikiliza mwalimu .
“ Nimeshuhudia leo hata wanafunzi watatu wakianguka kwa kuishia nguvu na baada ya kuwauliza wanasema hawajala chochote toka walipokula chakula usiku wa jana sasa hili si zuri sana mtoto anakuja shule bila hata kunywa chai na anashinda na njaa hadi anaanguka kwa kuishia nguvu kutokana na njaa “ alisema mkuu huyo wa mkoa
Kuwa lazima kila shule kupitia kamati zake za shule kuweka utaratibu wa kuwahamasisha wazazi kuchangia chakula ili kuanzisha utaratibu wa kula chakula shuleni na kuwa ambacho hataki kusikia ni wazazi kuchangishwa fedha za chakula .
“ Naagiza wazazi wote kuanza kuchagia chakula kwa ajili ya watoto wao wawapo shule na sitaki kusikia wazazi wakichangishwa fedha za chakula lazima muweke utaratibu wa kutengeneza bajeti ya chakula kwa kila mwanafunzi anatakiwa kuchangia mahindi na maharage kiasi gani ni vitu ambavyo kila mmoja anauwezo wa kuchangia na sio kulazimisha wazazi kuchangia fedha wengi hawana uwezo wa kutoa fedha ila chakula wanauwezo huo “
Katika hatua nyingine mkuu huyo wa mkoa alieleza kusikitishwa na kasi ya wanafunzi kupata mimba katika tarafa ya Mazombe kutokana na miezi miwili pekee wanafunzi 12 wa sekondari kukatisha masomo kutokana na tatizo la mimba hivyo kuagiza wale wote wanaohusika na mimba hizo kusakwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Hapi alisema sehemu kubwa sababu zinazochangia wanafunzi hao kupata mimba ni kukaa nje ya shule hivyo lazima kuwepo mpango wa shule ambazo hazina mabweni ya wanafunzi kuanzisha ujenzi wa mabweni lakini kuanzisha utaratibu wa kuwalinda watoto wa kike dhidi ya vijana wanaojihusisha na mahusiano na wanafunzi hao .
Aidha aliwataka viongozi wa tarafa ya mazombe likiwemo jeshi la polisi kufanya msako kwa wote wanaojihusisha kimapenzi na wanafunzi hao pamoja na kuwakamata wazazi ambao wanamalizana na watuhumiwa wa mimba za wanafunzi nje ya vyombo vya sheria.
Wakati huo huo Hapi ameagiza wanafunzi wote ambao walichaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari nab ado wapo mitaani kwa kisingizio cha kukosa sare za shule kuripoti shule wakiwa na nguo zao za nyumbani .
Alisema kuwa walimu wasiwazuie wanafunzi wasio na uwezo wa kununua sare za shule kuripoti shule kuanza masomo kwani sare haipaswi kuwa kikwazo cha watoto hao kusoma kuwa lengo la serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Magufuli kufuta ada ni kutaka watoto wote wasome na gharama kubwa serikali inagharamia elimu nchini .
Hivyo aliagiza wazazi ambao watoto wao wamefaulu na hawapo shule kukamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria kwani kitendo cha mtoto kulipiwa gharama na serikali kwa ajili ya kupata elimu na mzazi kushindwa kumpeleka mtoto shule ni sawa na uhujumu uchumi .
Awali mkuu wa shule ya Sekondari Mazombe Crispin Ngatunga alisema kuwa kutokana na tatizo la wanafunzi kuanguka njaa uongozi wa shule hiyo umekutana na wazazi na kuweka mpango wa kuanzisha utaratibu wa kuwapa chakula shuleni hapo mpango ambao utaanza wiki hii .
Kuhusu mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza alisema kuwa jumla ya wanafunzi 251 walipangwa katika shule hiyo kuanza masomo mwaka huu walioripoti ni wanafunzi 205 na wanafunzi 26 hawajaripoti hadi sasa .
Post A Comment: