Wednesday, 11 March 2020

RC HAPI AAGIZA VIJIJI VYOTE WILAYA IRINGA KUPATA UMEME KABLA YA JUNI 2020 ...

Mkuu wa mkoa wa Iringa Ally Hapi wa tatu kushoto akishirikiana na viongozi mbali mbali kukata utepe kuzindua umeme kijiji cha Lupembelwasenga leo.
.......................................................

MKUU wa mkoa wa Iringa Ally Hapi amemwagiza mkandarasi wa kampuni ya Sengerema anayesambaza umeme vijijini kuhakikisha unakamilisha usambazaji wa umeme kabla ya Juni mwaka huu.

Mkuu wa mkoa ametoa agizo hilo leo  wakati akizindua umeme katika vijiji viwili vya Lupembelwasenga na Igangidunu .

Alisema kuwa lengo la serikali ni kufanikisha usambazaji wa umeme vijijini na ifikapo mwishoni mwa mwaka huu 2020 vijiji vyote viwe vimefikiwa na huduma ya umeme na wananchi waweze kuondokana na kero ya matumizi ya vibatali .

"Natambua kampuni hii ya Sengerema inayosambaza umeme inafanya kazi chini ya wakala wa huduma za umeme vijijini (REA) sasa naagiza kasi ya usambazaji wa umeme iongozwe na vijiji  vyote sita vilivyosalia katika wilaya ya Iringa kabla ya Juni mwaka huu vijiji hivyo viwe vimepata umeme"

Hapi alisema hatahitaji kuona wananchi wa wilaya ya Iringa na mkoa kwa ujumla wanamaliza mwaka 2020 bila kuwa na nishati ya umeme .

Hata hivyo aliagiza kila mwananchi apewe umeme huo kwa bei elekezi ya Rais Dkt John Magufuli ya shilingi 27000 tu na sio zaidi ya hapo .

Alisema hataacha kuchukua hatua kwa mtumishi yeyote wa TANESCO ama REA ambae atatoza wananchi umeme zaidi ya shilingi 27000 iliyoelekezwa.


Pia alisema hakuna kikwazo chochote kwa mwananchi kuingiziwa  umeme hata kama anaishi katika nyumba ya nyasi ni haki yake kupelekewa umeme .

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa mkoa aliwataka wananchi wa Iringa kuendelea kushiriki katika ujenzi wa vyumba vya madarasa na nyumba vya walimu ili kuboresha mazingira ya elimu mkoani hapa.

Alishauri viongozi wa vijiji kuweka utaratibu wa kuwapa motisha ya mashamba ya kulima ama nyumba za kuishi walimu badala ya kuwaacha wajitegemee.

Alisema iwapo walimu watapewa motisha ya nyumba za kuishi na mashamba hawatatamani kuondoka katika shule za vijiji .

Awali mkuu wilaya ya Iringa Richard Kasesela alisema kuwa wilaya yake vijiji ambavyo havijafikiwa na umeme ni 4 na kabla ya Juni anaamini vijiji vitano vitakuwa na umeme ila kijiji cha Mapera  mengi ndicho kinaweza kuwa hakina umeme kutokana na Joghorafia yake hapo REA wanampango wa kupeleka umeme wa jua.

No comments:

Post a Comment