Monday, 2 March 2020

NAIBU KATIBU MKUU CCM TAIFA AWASHANGAA WANAOTAKA KUPIMANA UBAVU NA RAIS MAGUFULI 2020.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania bara Rodrick Mpogolo akimkabidhi cheti kada wa CCM wa Kibaha Mjini Christopher Mjema kutokana na kazi kubwa ya kukipigania chama ,hafla hiyo ilifanyika Machi 02 katika mkutano mkuu wa CCM Wilaya uliolenga kueleza utekelezaji wa ilani ya CCM ndani ya miaka minne iliyopita.picha na Gustaphu Haule

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi  (CCM)Tanzania bara Rodrick Mpogolo( kulia) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kugawa pikipiki 14 zenye thamani ya milioni 35 zilizotolewa na mbunge wa Kibaha Mjini Silvestry Koka (wa tatu kushoto)kwa makatibu wa Kata 14 na katikati ni mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini Maulid Bundala.picha na Gustaphu Haule
Na GUSTAPHU HAULE,PWANI

NAIBU katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania bara Rodrick Mpogolo,anawashangaa watu wanaotaka kupimana ubavu na Rais Dkt.John Magufuli kwa kutaka kugombea urais kwani wanajisumbua kwakuwa Magufuli ni mchapakazi anayependwa na Watanzania.

Aidha, Mpogolo amewashauri wapinzani wa kutoka nje ya chama na ndani ya chama wamuache Rais achape kazi kwani Watanzania wanaimani nae kubwa kutokana na kazi alizozifanya ndani ya miaka minne.

Mpogolo,alitoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM Kibaha Mjini uliofanyika kwa ajili ya kueleza namna ambavyo ilani imetekelezwa kwa muda wa miaka minne iliyopita.

Alisema Rais Magufuli,ameibadilisha nchi na sasa imekuwa imara kutokana na kufanya mambo ambayo yanaijenga nchi kiuchumi na hata katika sekta nyingine ikiwemo elimu,afya, miundombinu,Kilimo na mengineyo.

Mpogolo,alitaja baadhi ya miradi mikubwa iliyotekelezwa kuwa ni ujenzi wa reli ya kisasa ya mwendokasi,ujenzi wa bwawa kubwa la kufua umeme huko Wilayani Rufiji, ujenzi wa barabara za njia nane na miradi mingine mikubwa.

"Nawashauri wapinzani waliopo ndani ya chama na nje ya chama wamuache Rais achape kazi maana Watanzania wanaimani katika kujenga uchumi imara wa nchi yetu lakini nawashangaa wanaotaka kupimana ubavu na Rais kwa kutaka kugombea urais 2020 ,"alisema Mpogolo.

Amewataka wanaCCM kuendelea kuheshimiana na hata kuwaheshimu viongozi waliopo madarakani akiwemo Rais Magufuli na wabunge wa CCM akiwemo Silvestry Koka ili waendelee kufanyakazi za kuiletea maendeleo nchi yetu.

Katika mkutano huo mbunge wa Kibaha Mjini Silvestry Koka(CCM) ametoa msaada wa pikipiki 14 zenye thamani ya Sh .milioni 35 kwa ajili ya kuwasaidia makatibu Kata ili waweze kufanyakazi za kuimarisha chama pamoja na kutoa gari moja la wagonjwa.

Zoezi la kukabidhi pikipiki hizo lilifanywa na Naibu katibu mkuu Mpogolo muda mchache kabla ya kuzungumza na wajumbe hao ambapo alitumia nafasi hiyo kumpongeza mbunge huyo kwa harakati na juhudi zake za kununua vitendeakazi kazi hivyo.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi pikipiki hizo Koka,alisema kuwa lengo la kutoa pikipiki hizo ni kutaka kuimarisha Chama kupitia makatibu wa Kata na viongozi wengine wa Kata kwani alitambua namna ambavyo makatibu wanakabiliana na changamoto ya usafiri.

"Katika kuimarisha Chama Cha Mapinduzi (CCM ) Kibaha Mjini nimeona ni vyema tukawarahisishia kazi makatibu Kata 14 kwa kupata vitendeakazi ili kutatua changamoto za usafiri katika maeneo yao lakini hatahivyo bado tutaendelea kusaidia chama,"alisema Koka

Aidha,katika hatua nyingine Koka amekabidhi vitambulisho vya mabalozi wa Kibaha Mjini huku alisema pamoja na mambo makubwa yaliyofanyika bado ataendelea kushirikiana na Wananchi pamoja na wanaCCM wote katika kuleta maendeleo.

Kwa upande wake katibu wa CCM Kibaha Mjini Hafidu Luambano,alisema kuwa CCM ipo imara na wanaendelea kufanyakazi ya kujiandaa na uchaguzi mkuu kuanzia ngazi ya shina.

No comments:

Post a comment