Monday, 16 March 2020

KIJANA ANAYEKUNYWA MAJI LITA 100 KWA SIKU ATOA NENO .....


Kijana Msuha akinywa maji 
Mwanahabari Mtega akiwa Msuha
...............
  ERICK  MSUHA (47) mkazi wa Kijiji cha Narwanda kata ya Maguu Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma ambaye alikuwa anakunywa maji lita mia moja kwa siku(100)amevishukuru vyombo vya habari ikiwemo mtandao wa Msumba news kwa kuihabarisha jamii kuhusu ugonjwa wake na kumfanya apewe msaada wa matibabu.Mwandishi Amon Mtega anaripoti kutoka Mbinga Msuha akizungumza na Msumba  Nyumbani kwake Kijijini hapo amesema kuwa maradhi hayo yalimkuta baada ya kupigwa na radi mwaka 1993 na kumfanya aendelee kutaabika hadi  hadi alipoibuliwa na vyombo vya habari na kuwafanya wasamalia wema kutoka sehemu mbalimbali kumuwezesha kwenda kupatiwa matibabu.

  Amesema kuwa baada ya kufanikisha kwenda kupatiwa matibabu hayo katika Hospital ya Ikonda iliyopo Wilaya ya Makete mkoa wa Njombe hali yake ya kiafya  imeanza kutengamaa na sasa hanywi maji lita mia moja (100)kwa siku kama ilivyokuwa awali,na badala yake anakunywa chini ya lita 10.

 Amefafanua kuwa licha ya kuwa hivi sasa anatembea vizuri na kula vizuri  hata idadi ya unywaji maji imepungua na kumfanya anywe kiwango cha chini ya lita 10 na siyo kwa mara zote  tofauti na siku za nyuma kabla ya matibabu aliyoanza kupatiwa.

 "Navishukuru sana vyombo vya habari ikiwemo mtandao wa Msumba  kwa jitihada kubwa ya kuihabarisha jamii kuhusu ugonjwa wangu na hatimaye leo watu kwenye mapenzi mema wamenisaidia nasema asanteni sana " amesema Erick Msuha huku akitokwa na machozi ya furaha.“Nilikuwa napata mateso makali sana mali zote nimeuza kwaajili ya kujiuguza ,mke wangu niliyefunga naye ndoa Gerumana Ndunguru ,alinitoroka mzigo mkubwa ulikuwa kwa baba yangu mzazi Januari Msuha pamoja na mwanangu Porotas Msuha ambao walikuwa wakinihangaika kunichotea maji ya kunywa lita 100 kila siku”amesema Erick Msuha.

 Aidha amesema kuwa bado anaendelea na matibabu licha ya kuendelea vizuri kiafya na anatarajia kwenda tena katika Hospital ya Ikonda mwezi Mei 12 mwaka huu ,hivyo bado anaomba misaada juu yake iweze kufanyika ili akamalizie matibabu.

 Kwa upande wake mtoto Porotas (25)Msuha amesema kuwa  baba yake analeta matumaini ya kupona tofauti na awali hivyo anawashukuru watanzania wote wakiwemo wanahabari na umoja wa bonde la hagati lililopo Mbinga kwa umoja wao wa kuhakikisha baba yake anapatiwa matibabu.

“Kipindi cha Nyuma nilikuwa nashindwa  hata kwenda kufanya vibarua ili kukidhi mahitaji ya Nyumbani hapa ,hivyo hivyo kwa hali ninayoiona ya baba yangu sasa nitaweza kwenda kwenye vibarua kujitafutia riziki "amesema Porotasi Msuha.

  Naye baba mzazi , Januari Msuha (72)amesema kuwa mwanaye Erick Msuha ni mzaliwa wa kwanza kati ya watoto nane ambao baadhi yao hawajulikani waliko kiasi cha kushindwa kumjulia hali ndugu yao jambo ambalo lisema linamuumiza  sana ila cha kumshukuru Mungu ndugu yao anaendelea vizuri.

 Aidha kufuatia hali hiyo Erick Msuha aliyaweka mawasiliano yake wazi kama kuna mtu anahitaji kumsaidia awasiliane kwa No.0757-240221 na N0.0675-473105

No comments:

Post a comment