Wednesday, 4 March 2020

Dk. Shein Afurahishwa na ukuaji wa kiuchumi Zanzibar


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza jinsi alivyopokea kwa furaha taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya kuendelea kukua kwa uchumi wa Zanzibar.

Dk. Shein aliyasema hayo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga ambapo katika mazungumzo hayo Cavana huyo alimueleza Dk. Shein jinsi uchumi wa Zanzibar unavyoendelea kuimarika.

Katika maelezo hayo Rais Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa hiyo ni habari njema ambayo inatoa mwanga wa maendeleo ya uchumi hapa Zanzibar kwani juhudi za makusudi bado zinaendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha uchumi unaimarika.

Rais Dk. Shein aliongeza kuwa hatua hiyo imefikiwa kutokana na uwepo wa uongozi bora sambamba na mashirikiano mazuri yaliopo kati ya Serikali, wananchi pamoja na  na Benki kuu ya Tanzania (BoT).

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza kuwa katika suala zima la mfumko wa bei pia, amepokea kwa furaha  maelezo ya kuwa mfumko wa bei uko vizuri hapa nchini hali ambayo inaleta faraja kwa wananchi.

No comments:

Post a comment