Wednesday, 25 March 2020

DC KATAMBI ALIAGIZA JIJI LA DODOMA KUMALIZA CHANGAMOTO YA TAKATAKA NDANI YA SAA 72


 Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi akikatiza ndani ya Soko la Sabasaba kujionea hali ya usafi ambapo ameagiza Jiji la Dodoma na viongozi wa Soko hilo kutengeneza mfumo mzuri wa ufanyaji usafi ili kuweka mazingira katika hali nzuri.
 Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe Patrobas Katambi akiwa kwenye dampo lingine ambalo uchafu umekaa bila kuondolewa kwa muda wa miezi mitatu. DC Katambi ametoa saa 72 kwa Jiji la Dodoma kumaliza changamoto hiyo.
 Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi akiwa kwenye mojawapo ya dampo bubu eneo la Chamwino ambalo uchafu umekusanywa bila kuondolewa jambo ambalo linahatarisha afya za wakazi wa eneo hilo.
 Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi (mwenye shati la kijani) akitoa maelekezo kwa maafisa mazingira wa Jiji la Dodoma na viongozi wa Soko la Majengo baada ya kutembelea soko hilo kukagua machinjio ya Kuku ambapo hajaridhishwa na hali ya usafi wa soko hilo.

KATIKA kuepukana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa Kipindupindu, Jiji la Dodoma limeagizwa kuchukua hatua za haraka kwa kumaliza changamoto ya uchafu ambayo imekua ikilalamikiwa na wananchi wake.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe Patrobas Katambi leo wakati alipofanya ziara ya kukagua usafi wa mazingira katika mitaa na masoko mbalimbali ya jiji hilo.

Katika ziara yake hiyo, DC Katambi amebaini uwepo wa takataka nyingi kwenye mitaa ambayo ni makazi ya watu jambo ambalo linahatarisha afya zao haswa watoto wadogo.

DC Katambi ametoa saa 72 kwa Jiji hilo kuhakikisha linamaliza changamoto hiyo kwa kuweka mitaa Katika hali ya usafiri ikiwa ni pamoja na kutoa takataka zote na kama hawatofanya hivi atawachukulia hatua kali za kinidhamu.

" Hali ni mbaya nimetembelea maeneo mbalimbali leo, nimeenda Chamwino, Bonanza ukienda mtaa wa Nduka na pia Kisasa kwenye barabara mbili utakuta madampo ambayo yamejazana yakiwa na uchafu mwingi sana.

Wananchi wanapiga simu wanalalamika wanatoa pesa lakini uchafu hauondolewi, sasa hii Kampuni mlioipa kazi ya kuzoa taka kama imeshindwa imeshindwa basi nitaifutilia mbali kwa sababu kuna changamoto kubwa sana aidha haina uwezo au usimamizi ni mbovu, sasa sipo tayari kuona wananchi wangu wanapata magonjwa na mimi nipo," Amesema DC Katambi.

Amesema suala la changamoto ya takataka kwenye jiji kama wasipochukua hatua za haraka basi kuna hatari ya kuwepo kwa magonjwa ya mlipuko hasa katika kipindi hiki cha mvua.

" Agizo langu la kwanza kwenu Jiji ni kuhakikisha hiyo Kampuni ya Greenwaste mnaifanyia usahili upya kwa kufanya mapitio ya makubaliano, kwa sababu kuna shida na mambo hayaendi vizuri kwa sababu malalamiko ya wananchi yamekua mengi.

Angalia mapato na jinsi gani ndani ya kipindi chote mmefanya kazi kwa maana ya mwenendo na mniletee taarifa tuweze kuangalia idadi ya magari waliyonayo na maeneo wanayofika lakini pili Jiji na vikundi kazi mkae na mpange mkakati wa kumaliza changamoto ya uchafu Dodoma," Amesema Katambi.

DC Katambi amesema ndani ya saa 72 ambazo ametoa kwa Jiji hilo ni kuhakikisha takataka zote zinaondolewa na kupelekwa eneo linalotakiwa pamoja na kumpelekea mpango kazi ili kuona namna gani wanaweza kumaliza changamoto hiyo.

No comments:

Post a Comment