Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesitisha shughuli zenye mikusanyiko ya watu wengi, ikiwa ni hatua za kudhibiti kuenea kwa virusi vya Corona
 
Ugonjwa huo ulioanzia katika mji wa Wuhan, China Desemba, 2019 na baadaye kuanza kusambaa nchi mbalimbali umesababisha vifo vya watu zaidi ya 4,500 huku Tanzania ikiwa nchi ya tatu Afrika Mashariki kuwa na mgonjwa wa corona baada ya Kenya na Rwanda.

Agizo hilo limetolewa leo tarehe 17 Machi 2020 na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.
 
Amesema, mikutano yote ikiwemo ya ndani na hadhara yenye asili ya mikusanyiko ya watu wengi, itasimama hadi pale chama hicho kitakapotoa maagizo mengine.

“CCM taasisi kubwa, kinazo shughuli zake zinazoendelea kutoka mwanzo hadi mwisho wa mwaka, matukio makubwa ya ujenzi wa chama ya nje na ndani ya jamii.

“Maelekezo shughuli zote za CCM zenye asili ya mikusanyiko mikubwa, iwe ya ndani au ya hadhara. Shughuli hizo zisitishwe mara moja kuanzia leo,” amesema Polepole.

Polepole amesema ziara za viongozi wa chama hicho zilizokua zimeanza au zinazoratarajiwa kufanyika zitasimama kuanzia leo, hadi pale hali itakapokua shwari.

Aidha, Polepole amekosoa uamuzi wa Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alioutoa jana tarehe 16 Machi 2020, kwamba wataanza mikutano ya hadhara Aprili mwaka huu.

“ Freeman Mbowe anahamasisha watu kufanya mikutano ya hadhara hapa Watanzania mpime nani anawapenda, nani anataka kuwatumia.

"Corona inauwa kweli na ukiipata ni rahisi kuambukiza wengine na eneo rahisi kuambukizana ni kwenye mikusanyikon,”  Amesema  Polepole
Share To:

msumbanews

Post A Comment: