Wednesday, 5 February 2020

RC HAPI ATAHADHARISHA WANANCHI JUU YA MVUA ,ATAKA WALEVI KUPUMZIKA AMA KUPUNGUZA POMBE


Mkuu wa mkoa wa Iringa Ally Hapi akiongoza kamati yake ya ulinzi na usalama kukagua madhara ya mvua Ilula 
Mkuu wa mkoa wa Iringa Ally Hapi na mkuu wa wilaya ya Kilolo Asia Abdallah wakitazama barabara iliyoharibiwa na mvua eneo la solo la mbuzi Ilula barabara kuu ya Iringa -Dar es Salaam 
Meneja wa TANROAD mkoa wa Iringa akimwelekeza mkuu wa mkoa na kamati yake barabara iliyoharibiwa 
Sehemu ya barabara iliyoharibiwa na mvua 
Mkuu wa mkoa wa Iringa Ally Hapi akiangalia nyumba zolizobomoka kwa mafuriko Ilula 
Mkuu wa mkoa wa Iringa Ally Hapi na mkuu wa wilaya ya Kilolo Asia Abdallah na kamati ya ulinzi na usalama wakitazama madhara ya mvua Ilula 

Mkuu wa mkoa wa Iringa Ally Hapi amewataka wananchi wa mkoa huo kuchukua tahadhari ya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha ikiwa ni pamoja na wale wanaolewa kupita kiasi kupunguza pombe ili kuepukana na kusombwa na mafuriko pindi wakiwa hawajitambui kwa ulevi .

Akizungumza na wananchi wa Ilula wilaya ya Kilolo wakati wa ziara yake  na kamati ya ulinzi na usalama mkoa alipokagua madhara ya mvua hiyo katika Mji wa Ilula February 4 /2020 ,Hapi alisema ni vizuri wakati serikali ikiendelea kuchukua tahadhari kwa kuboresha miundo mbinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua hizo pia wananchi nao waziri kujihadhari na mvua hizo.

Alisema wapo baadhi ya watu wamekuwa na Utamaduni wa kulewa kupita kiasi ni vizuri kwa kipindi hiki kupunguza pombe ama kununua pombe na kunywea nyumbani .

"Kati ya vifo vitatu vilivyojitokeza matukio ya ulevi kupita kiasi yamechangia vifo hivyo kwa mtu kulewa na wakati anarudi nyumbani anakutana na maji na kwa kuwa kulewa anajaribu kupima urefu wa maji hayo kwa kuingiza mguu na matokeo yake anachukuliwa "

Hivyo alisema ili kuepuka majanga hayo ni vema kupunguza ulevi ama kununua pombe na kunywea nyumbani katika mazingira salama .

Pia aliwaonya wananchi kuepuka kunywa maji yasiyochemshwa kwani maji hayo si salama kutokana na vyoo vingi kufurika hivyo vinyesi vya binadamu vinasafirishwa na maji hayo na ni rahisi kupata kipindupindu.

Akizungumzia madhara yatokanayo na mvua hizo alisema ni pamoja na uharibifu mkubwa wa miundo mbinu ya barabara katika wilaya hiyo ya Kilolo na Iringa pia nyumba kadhaa kusombwa na mafuriko na hivyo ameagiza watendaji wa serikali za vijiji na mitaa kupita nyumba kwa nyumba kukagua ubora wa nyumba hizo na zile zilizokwenye hatari ya kubomoka basi wasaidie kuwahamisha wananchi hao kwa kuwaelimisha kwanza.

Kwani alisema baadhi ya nyumba hasa za uongo zimekuwa zikionesha dalili zote za kuanguka hivyo ni vizuri kuwatafutia mazingira salama wale wanaoishi kwenye nyumba hizo.

Katika katika hatua nyingine mkuu huyo wa mkoa ameagiza kukamatwa kwa wananchi watakaobainika wakiwaficha watuhumiwa wa makosa ya ubakaji na ulawiti watoto .

Hapi alitoa agizo hilo kufuatia taarifa iliyotolewa na mkuu wa wilaya ya Kilolo Asia Abdallah kuhusiana na tukio la mwanaume mmoja mjini Ilula kukamatwa kwa tuhuma za kuwabaka watoto zaidi ya watano wenye miaka kati ya miwili na saba .
Alisema kuwa hatakubali kuona matukio ya ukatili wa kijinsia yakiendelea kuongezeka katika mkoa wa Iringa na watuhumiwa wakimalizana na ndugu wa watoto hao .

Kwani alisema kwa mwaka jana  pekee matukio zaidi ya 400 yameripotiwa ndani ya mkoa kwa watoto kulawitia na kubakwa huku wazazi wakimalizana na watuhumiwa kwa kupeana pombe ya ulanzi na fedha.

Pamoja na kutangaza kuwachukulia hatua wazazi watakaokubali kumalizana na watuhumiwa wa makosa hayo pia alisema hatasita kuchukua hatua dhidi ya askari wala rushwa ambao wamekuwa wakiwaficha watuhumiwa hao .

Wakati huo huo mkuu wa mkoa amempongeza na kumzawadia pesa mkuu wa kituo cha Ilula Siamon Kitana kwa kazi nzuri ya kuwahudumia wananchi wanaofika kituoni hapo kulalamika na kutaka askari wengine kuiga mfano huo na sisite kuchukua hatua dhidi ya askari wazembe na wala rushwa.

No comments:

Post a comment