Saturday, 4 January 2020

MWANAMKE MATATANI KWA TUHUMA ZA WIZI WA WATOTO MBEYA

Jeshi Ia Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mwanamke mmoja aitwaye ,Hawa Ally (40)Mkazi wa Tegeta Jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kukutwa na watoto wadogo wawili wakazi wa Ituha  Jijini Mbeya.Mwandishi Esther Macha anaripoti toka Mbeya 

Watoto waliokutwa  na mwanamke huyo wametajwa kwa majina kuwa ni  ,Faisal  Juma (05)Farhana Juma mwaka mmoja na miezi mitano ambao walichukuliwa na mwanamke huyo wakiwa wanacheza nje ya nyumba yao Desemba 28 mwaka jana. 

Akizungumza na waandishi wa habari Jana Kamanda wa polisi Jijini Mbeya, Ulrich Matei alisema kuwa watoto hao walichukuliwa na mwanamke huyo wakiwa wanacheza nje ya nyumba yao huko mtaa wa Shewa Ituha Jijini hapa. 

Matei alisema kuwa mwanamke huyo alikamatwa Januari Mosi, 2020 huko Wilayani Nzega Mkoani Tabora baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa za kuwepo kwa mama huyo akiwa na watoto wawili ambao alisafiri nao hadi mkoani Tabora akitokea Jijini  hapa Mbeya.


Aidha Kamanda Matei alisema desemba 28 mwaka jana majira ya saa 14.00  mchana baba mzazi wa watoto hao Mashaka Juma aligundua kupotea kwa watoto wake wawili. 

Baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa hizo, lilianza msako mara moja ikiwa ni pamoja na kufanya mawasiliano na mikoa mingine na kufanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa akiwa na watoto hao wakiwa hai. 


No comments:

Post a comment