Friday, 20 December 2019

HUDUMA ZA AFYA NCHINI KUBORESHWA   Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto , Ummy Mwalimu akizungumza na wagonjwa Hospitali ya Rufaa ya Tabora 

   Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto , Ummy Mwalimu akifanya ukaguzi wa Hospitali ya Tabora 

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imedhamiria kuboresha huduma za Rufaa katika Hospitali za Rufaa za mikoa kwa kuhakikisha inaboresha kwa kujenga miundombinu ya majengo ya dharura na ajali.mwandishi Rayson Mwaisemba WAMJW anaripoti toka Tabora .

   Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto , Ummy Mwalimu wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora.

" Sisi kama Serikali, tumedhamiria kuboresha huduma za Rufaa katika Hospitali za Rufaa za Mikoa, kwa kuhakikisha tunaweka miundombinu, hususan jengo la dharura na ajali ". alisema Waziri Ummy Mwalimu.

Hata hivyo, Waziri Ummy alisema Serikali imedhamiria kuboresha huduma za Afya kwa wananchi, kwa kutenga takribani Bilioni 8.8 kwa ajili ya ujenzi wa zaidi ya Vituo vya Afya 13, huku akieleza kuwa Hospitali za Wilaya za Sikonge na Uyui nazo zinaendelea kujengwa hali itakayosaidia kupunguza mzigo kwa Hospitali ya Mkoa.

"Sisi kama Serikali tumedhamiria kuboresha huduma za Afya, kuanzia miundombinu, Serikali tunajenga vituo vya Afya zaidi ya 13, ambayo takribani Bilioni 8.8 zimeshaingizwa na vingine nimeanza kutoa huduma lakini tunajenga Hospitali mbili za Wilaya ambazo ni Sikonge pamoja na Uyui" alisema

Licha ya kupunguza kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa Malaria nchini, Waziri Ummy ameagiza kupitia Maafisa Afya kutoa elimu kwa wananchi ili kutokomeza mazalia ya mbu waenezao Malaria, huku akisisitiza kuwa ni lazima Halmashauri kununua viuadudu vya kuangamiza viluilui katika mazalia ya mbu.

Mbali na hayo, Waziri Ummy aliipongeza timu ya Afya ya Mkoa kwa jitihada inazozichukua katika kuimarisha usafi wa mazingira hususan katika ujenzi na matumizi ya vyoo bora jambo litalosaidia kupunguza magonjwa ya kuhara, magonjwa ya tumbo na Kipindupindu.

"Ujenzi na matumizi ya vyoo Bora ndani ya mwaka mmoja mmetoka Asilimia 53.7 mpaka asilimia 59, lakini pia tumepunguza kaya ambazo hazina vyoo kabisa kutoka asilimia 7 mpaka asilimia 2" alisema.

Kwa upande mwingine, ameagiza asilimia 2 ya watu wasiokuwa na vyoo kutafutwa ili kuhakikisha wanajenga vyoo na kuvitumia kwa usahihi, huku akisisitiza wasiofanya hivyo ndani ya muda wa makubaliano wachukuliwe hatua za kisheria, alisisitiza.

Pia, Waziri Ummy alisema kuwa katika Mkoa wa Tabora vifo vya akina mama wajawazito vimepungua kutoka wajawazito 99 mpaka wajawazito 60 kwa mwaka huku akisisitiza Watoa huduma kuendelea kujituma ili kuhakikisha usalama wa mama na mtoto.

Aliendelea kusema, Wanawake ambao wanajifungulia katika vituo vya kutolea huduma za Afya katika Mkoa wa Tabora ni zaidi ya Asilimia 100%, huku kitaifa ikiwa ni asilimia 63, hivyo ametoa Wito kwa wanawake kuendelea kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za Afya.

"Tumeona kwamba Wanawake ambao wanajifungulia katika vituo vya kutolea huduma za Afya katika Mkoa wa Tabora ni zaidi ya 100%, wakati kitaifa tunazungumizia asilimia 63 kwahiyo hongereni sana kwa kupunguza vifo, kutoka wajawazito 99 mpaka 60" alisema

No comments:

Post a comment