Abdul Nondo kushoto akizungumza na wakili wake Jebra Kambole ambae ni mmoja wa mawakili wa mtandao wa watetezi wa haki za binadamu Tanzania (THRDC) waliompigania kisheria
Na Francis Godwin,Iringa
ALIYEKUWA mwenyekiti mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP) Abdul Omary Nondo ambae alikuwa ameishinda jamhuri katika kesi ya kudaiwa kujiteka na kutuma taarifa za uongo leo ameshinda tena rufaa iliyokuwa imekatwa na jamhuri dhidi yake .
Katika maamuzi hayo jamhuri imeshindwa kuithibitishia mahakama kuu kulingana na sababu za rufaa zilizoletwa na Jamhuri huku mahakama kuu kanda ya Iringa imefikia kumwachia huru Nondo baada ya kujiridhisha kwamba upande wa serikali ulijielekeza vibaya kwa kukimbilia kufungua kesi dhidi ya mlalamikaji badala ya kushughulikia malalamiko yake kwa jeshi la polisi.
Rufaa ya Nondo imetolewa hukumu na jaji wa mahakama kuu kanda ya Iringa Panterine Kente ambapo katika maelrezo yake wakati wa kutoa hukumu hiyo alisema hati ya maelezo (caution statement) iliyoletwa mahakamani haikuwa ushahidi tosha kwa jamhuri kwa kuwa ilikuwa na majina tofauti na majina yaliyopo kwenye hati ya mashataka.
Kutokana na hukumu hiyo ya kumwachia huru Nondo sasa anakuwa ni raia huru katika nchi baada ya hukumu hiyo ya mahakama .
Akizungumza baada ya kuachiwa huru kwa mara ya pili sasa Nondo amemshukuru Mungu kwa kusimama upande wake pia amepongeza watanzania wote ambao walikuwa wakimwombea wakati wote pamoja na mtandao wa watetezi wa haki za binadamu Tanzania (THRDC) kwa kumpigania hadi mwisho .
Nondo ambaye awali alishtakiwa katika mahakama ya wilaya Iringa alishtakiwa kwa kosa la kutoa taarifa za uongo kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa Mtandaoni, 2015 ambapo aliushinda upande wa jamhuri kwakuwa Jamhuri ilishindwa kuthibitisha paspo shaka malalamiko waliyoleta mahakamani
Post A Comment: