Na Ahmed Mahmoud,Arusha
Maafisa wawili wa halmashauri ya jiji la Arusha wamesimamishwa kazi kutokana na tuhuma za kuihujumu halmashauli hiyo kwenye mradi wa mchakato wa ujenzi wa kituo kikuu cha Mabasi  jijini hapa.

Akiongea na vyombo vya habari ofisini kwake Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dkt Maulid Madeni aliwataja watumishi hao kuwa ni Mkuu wa idara ya Mipango miji na Ardhi,Dickley Nyato na Anne Mwambene ambaye ni Mchumi wa jiji hilo.

Dkt Madeni amesema kuwa Nyato anatuhumiwa ameidanganya halmashauri hiyo kuhusu kiwanja namba 6 kilichopo Oljoro chenye hati namba 10 kinachojengwa kituo cha mabasi kuwa hati yake imemalizika tangu mwaka 1982

Alisema jambo hilo si sahihi kwani hati ya eneo hilo imetolewa tangu mwaka 1949 na  itadumu kwa miaka 99 na kumalizika mwaka 2048

Alisema lengo la Mkuu huyo wa Idara ni kutaka kuiuzia halmashauri huyo eneo hilo kwa bei kubwa na kujipatia fedha kwa kushirikiana na mafisadi kinyuma na utaratibu.

Pia mkurugenzi huyo anamtuhumu Nyato kuishawishi halmashauri hiyo iwalipe fidia  ya sh,Bilioni 1.9 badala ya bilioni 1.1 wakazi wa eneo la Olasiti waliokubali kupisha eneo lao lenye ukubwa wa ekari 29 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha mabasi.

Dkt. Madeni ameongeza kuwa nafasi ya Nyato itakaimiwa na kaimu wake Solomon Lukumay
Katika hatua nyingine Dkt Madeni amemsimamisha kazi mchumi wa jiji hilo ,Anne Mwambene kwa kushindwa kutoa maelezo ya kutoka kuhusu mradi wa ujenzi wa kituo hicho cha mabasi na kusababisha mradi huo kuchelewa kuanza .

Dkt Madeni amesema kuwa nafasi ya Mwambene itakaimiwa na Mathias Shindika wakati uchunguzi wa suala lake ukiendelea .

Amesema  wakati akisubiri uchunguzi wa tuhuma hizo atatakiwa kuripoti kila ijumaa ya kila wiki kwa mwajiri wake na kwamba hatatakiwa kusafiri nje ya nchi na mkoa wa Arusha wakati akisubiri hatua zingine kuchukukuwa.

Dkt Madeni amesema kuwa ataendelea kusimamia na kuona wananchi wanapata huduma bora hivyo kuwataka watendaji chini yake kuhakisha wanafanyakazi zao kwa kufuata sheria kanuni na taratibu za kazi na pia kuacha majungu.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: