Monday, 18 November 2019

Vyuo vikuu nchini vyatakiwa kuwaandaa Vijana kulingana na mahitaji ya sokoHappy Lazaro,Arusha.

Arusha.Mwanasheria mkuu wa  serikali  Adelardus  Kilangi amevitaka vyuo vikuu nchini kuwaandaa  Vijana kulingana na mahitaji ya soko la ajira ili kuweza kuondokana na changamoto ya kukaa mitaani pindi watakapohitimu .

Aliyasema hayo Jana wakati akizungumza katika  mahafali ya nne ya chuo kikuu cha mtakatifu Augustine Tanzania tawi la Arusha ambapo jumla ya wanafunzi  498 walihitimu kozi mbalimbali.

Kilangi alisema kuwa,umefika wakati Sasa wa vyuo vikuu kuhakikisha vinawaandaa Vijana kulingana na mahitaji ya soko ili waweze kupata ajira kwa haraka  pindi watakapohitimu .

 "Mimi naviomba vyuo kuanza kujiuliza  kwa nini vijana wanaomaliza  hawajiajiri ama kuajiriwa  kwa kuzifuata fursa mbalimbali zilizopo nchini ikiwemo kwenye sekta ya  kilimo jambo ambalo wanatakiwa kulitatua ili kuleta mabadiliko."alisema .

Alisema kuwa ,wahitimu wanapaswa kuangalia ni kwa jinsi gani watazitambua na kuzitumia fursa mbali mbali za kukuza maendeleo ya nchi kwa kutumia taaluma zao na kuwa washindani katika soko la ajira kwa kufungua fursa za kujiajiri wenyewe.

“tumieni muda wenu na elimu mliyoipata kuzitafuta fursa katika mitandao ya kijamii na kuacha kutumia mitandao hiyo kwa mambo yasiyofaa kwa kuwa soko kubwa lipo ndani ya mitandao hiyo”alisema Kilangi.

Awali Mkuu wa wilaya ya  Arusha Fabian Daqarro alivitaka vyuo mbalimbali kuandaa mitaala ya masomo kulingana na mahitaji ya soko la ajira ndani na nje ya nchi na hiyo itapunguza changamoto ya Vijana wengi kukaa mitihani kwa muda mrefu wakisaka ajira.

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa jimbo kuu katoliki Arusha ,Isaack Amani alisema kuwa,katika kipindi hiki ambacho Kuna changamoto kubwa ya ajira hususani kwa Vijana Kuna umuhimu mkubwa kwa wahitimu hao kutanguliza weledi na nidhamu mbele ili waweze kukabiliana na ushindani uliopo.

Aidha aliwataka wahitimu watumie talanta zao na vipawa kusukuma maendeleo ya Taifa mbele huku wakiendana na dhana ya uchumi wa viwanda .

Naye Mkurugenzi wa  chuo hicho cha Arusha,Charles Rufyiliza alisema kuwa, kuna dhana imejengeka kuwa wanao soma vyuo vya binafsi hawapati mikopo kutoka Serikalini dhana hiyo sio kweli kwani wanafunzi walioomba mikopo mwaka huu pesa zao zimefika kabla wao hawajaripoti chuoni.

Nao baadhi ya wahitimu, Nashukuru Sanga na Freedom Kishokera walisema kuwa, watatumia elimu waliyoipata kujiajiri na kutumia fursa  za ajira zilizopo  ndani na nje ya nchi.Mwisho.

No comments:

Post a comment