Friday, 15 November 2019

USAJILI KILI MARATHON WAANZA KWA KASI

Washiriki wa mbio za kilometa 42 za Kilimanjaro Premium Lager marathon wakiwa tayari kuanza mashindano hayokatika mbio zilizopita. Usajili wa mashindano hayo umeanza kwa kasi kwa njia ya mtandao na Tigopesa.

Usajili wa mbio za 18 za Kilimanjaro Premium Lager Marathon, Tigo km 21 na Grand Malt Km 5 umeanza kwa kasi huku ukiwa juu kwa asilimia 30 ikilinganishwa na wakati kama huu mwaka jana. Hili ni ongezeko la asilimia 10 ndani ya wiki moja. 

Taarifa iliyotolewa na waandaaji wa mbio hizo ieeleza kuwa mwendendo ni mzuri na wamewataka washiriki kuchangamkia punguzo la bei litakalodumu hadi mwezi Januari mwakani. Washiriki wanajisajili kwa kupitia www.kilimanjaromarathon.com na kwa Tigopesa kwa kubonyeza *149*20#.

Mkurugenzi wa Mbio hizo nchini, John Bayo alisema kwa kupitia taarifa hiyo kuwa kuna idadi maalumu ya washiriki inayotakiwa kwa mbio zote tatu (Kilimanjaro Premium Lager Km 42, Tigo km 21 na Grand Malt Km 5) ili kuhakikisha kuw ambio hizo zinaendana na viwango vya Shirikisho la Kimataifa la Riadha (IAAF) ili kuhakikisha usalama unazingatiwa.

Kwa mujibu wa Bw. Bayo, hii pia itahakikisha washiriki wanafurahia mbio hizo bila ya msongamano na pia kutoa nafasi kwa waandaaji waweze kutoa huduma zinazotakiwa katika njia ya mashindano na sehemu ya kumalizia pia.

Kuhusu punguzo la bei, waandaaji hao pia walitoa wito kwa washiriki wachangamkie utaratibu huo ambao ulianza Oktoba Mosi 2019 hadi Januari 14 , 2020. Kwa raia wa Tanzania na wale kutoka nchi za Afrika Mashariki watalipa Tsh 15,000 kwa mbio za Km 42 na 21 na Tsh 5000 kwa km 5 lakini kuanzia Januari 15, 2020 hadi Februari 16, 2020 washiriki watakaojisajili watalipa Tsh 20,000 kwa km 42 na 21 na Tsh 5000 kwa km 5. 

Kwa wageni wakazi au wenye vibali vya kuishi na kufanya kazi na wale wa nchi za SADC watalipa USD 35 kwa km 42 na 21 na USD 5 kwa km 5 kuanzia Octoba 1, 2019 hadi Januari 14, 2020 lakini kuanzia Januari 15, 2020 hadi Februari 16, 2020 wanaojisajili watalipa USD 45 kwa km 42 na 21 na USD 5 kwa km 5. 

Washiriki wa kimataifa watalipa USD 70 kwa km 42 na 21 na USD 5 kwa km 5 kuanzia Oktoba 1, 2019 hadi Januari 14, 2020 na kuanzia Januari 15 hadi Februari 16, 2020 watalipa USD 85 kwa km 42 na Km 21 na USD 5 kwa km 5. 

Kwa mujibu wa waandaaji hao, usajili utafungwa rasmi saa sita usiku Februari 16, 2020 au pale ambapo idadi inayotakiwa itatimia.

Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka Chama Cha Riadha Tanzania, Baraza la Michezo Tanzania, Bodi ya Utalii Tannzania na wadau wengine wa riadha.

Washiriki pia walikumbushwa kuhusu vituo vya kuchukulia namba zao za ushiriki ambapo kwa Dar es Sallaam ni Mlimani City kuanzia February 22-23, 2020, Arusha ni Hoteli ya Kibo Palace kuanzia Februari 25-26 na Moshi ni Hoteli ya Keys kuanzia Februari 27-28. “Washiriki watatakiwa kujitambulisha na kuthibitisha kuwa wameshalipia kabla ya kukabidhiwa namba zao,” ilisema taarifa ya waandaaji. 

Wadhamini wa mbio za Kilimanjaro Marathon 2020 ni Kilimanjaro Premium lager, Tigo, Grand Malt Kilimanjaro Water, TPC Limited, Simba Cement, Barclays Bank na watoa huduma rasmi ni Kibo Palace Hotel, Keys Hotel, GardaWorld Security, Precision Air na CMC Automobiles.

Mashindano ya Kilimanjaro Marathon yanayoandaliwa na Wild Frontiers na kuratibiwa kitaifa na kampuni ya Executive Solutions, yanatarajiwa kufanyika Machi 1, 2020 katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi.

Washiriki wa mbio za Tigo kilometa 21 wakianza mbio hizo.

No comments:

Post a comment