Ferdinand Shayo,Killimanjaro.

Wananchi wa  Wilaya za  Moshi Vijijini  na Manispaa ya Moshi wametakiwa kushiriki katika vita ya kutokomeza udumavu miongoni mwa watoto wa wilaya hiyo kwa kulima mboga mboga na matunda na kuzitumia vizuri ili kuhakikisha kuwa watoto hawapati udumavu  na wanakua  vizuri kimwili na kiakili.

Mratibu wa Mradi wa Lishe unaotekelezwa na Shirika lisilokua la kiserikali la Initiative for Youth  ,Laurent Sabuni alisema hayo  wakati akitembelea klabu za lishe zilizoundwa mashuleni katika wilaya hizo ambazo zimelenga kuhamasisha ulimaji wa bustani za mboga mboga na kutumia mboga kwa wingi pamoja na vitamin ili kuondokana na tatizo la lishe duni .

Sabuni alisema kuwa wilaya hizo zinakabiliwa na tatizo la udumavu kwa watoto licha ya wazazi wao kuwa wakulima wazuri wa mboga na matunda ambayo mara nyingi wanauza na kupata fedha huku wakisahau kuwapa watoto wao lishe hiyo muhimu kwa ajili ya ujenzi wa afya ya akili na mwili.

“Tunafanya kampeni ya lishe katika kata 6 za Wilaya ya Moshi vijijini  na Manispaa ya Moshi ambazo ni Mabogini,Matala,Masaera,Kilimaposo na   Makuyuni huko tunafika katika vijiji kuelimisha juu ya namna ya kuandaa lishe bora kwa familia na watoto ,pia tumeunda klabu za lishe mashuleni ambazo tunatoa elimu kwa kushirikiana na Maafisa Lishe ili kutokomeza tatizo la udumavu” Alisema Sabuni

Hata hivyo Sabuni alifafanua kuwa ushirikishwaji wa wananchi umekua ukifanyika  kwa kuwafikia wananchi kupitia mikutano ya vijiji na kutembelea kaya kwa kaya hususan kaya ambazo ziko hatarini kupata tatizo la udumavu ili kuwanusuru.

Kwa upande wake Mtaalamu wa Lishe kutoka shirika hilo,Elias Joel alisema kuwa  wamekua wakitoa elimu juu ya uandaaji wa mboga na matunda ili  yasipoteze virutubisho muhimu vinavyohitajika kwenye mwili juhudi  ambazo tayari zimeanza kuzaa matunda kwa wananchi hususan kinamama wameanza kuwa na mwamko juu ya namna ya kuandaa lishe bora hivyo tunawashukuru wafadhili wa mradi ambao ni shirika la Global Alliance for improved nutrion gain kwa kutuwezesha kuwafikia wananchi na kupata matokeo mazuri.

Elly alisema kuwa katika kuhamasisha kilimo cha mboga mboga na matunda kama njia ya kupambana na umasikini pamoja na kukabiliana na changamoto ya lishe duni pia wamekua wakishirikiana na chama cha wakulima wa mboga mboga na matunda kinachofaamika kama TAHA ambao ni wataalamu na washauri wazuri wa masuala ya kilimo na lishe.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: