Thursday, 17 October 2019

Wafanyabiashara Manyara Wakunwa Na Utendaji Wa Rais Magufuli-waahidi Kulipa Kodi Kwa Hiari

Na Benny Mwaipaja, WFM, Manyara
WAFANYABIASHARA mkoani Manyara, wameahidi kuendelea kulipa kodi kwa hiari baada kuridhishwa na utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Wafanyabiashara hao wamemweleza Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji aliyekutana nao Mjini Babati ili kujadili fursa na changamoto zinazoikabili sekta binafsi pamoja na kuwaelimisha namna Serikali ilivyofuta kodi lukuki kwa lengo la kuwawezesha kufanyabiashara zao kwa tija Zaidi.

Pamoja na ahadi hiyo ya kulipa kodi kwa hiari, wafanyabiashara hao wamemwomba Dkt. Ashatu Kijaji awasaidie kufikisha kilio chao kwa Serikali ili idadi kubwa ya taasisi za Serikali zinazowabana kulipa kodi zipunguzwe, ama kodi zinazodaiwa ziunganishwe ili kumwondolea mfanyabiashara adha ya kudhibitiwa na Mamlaka nyingi.

Baadhi ya Mamlaka zilizotajwa ni pamoja na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Wakala wa Usalama Mahali pa Kazi (OSHA) na nyingine nyingi ambazo wamesema mbali na kuwatoza kodi kubwa lakini wamekuwa wakipata usumbufu wa aina mbalimbai.

Akijibu hoja mbalimbali za wafanyabiashara hao, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji amewapongeza wafanyabishara hao kwa kulipa kodi ambayo imeiwezesha Serikali kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya.

“Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii, mwezi Septemba, tumekusanya Zaidi ya shilingi trilioni 1.76 kiasi ambacho hakijawahi kutokea tangu nchi ipate uhuru” alisema Dkt. Kijaji

Alisema kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya ufanyajibiashara ambapo mpaka sasa imeondoa Zaidi ya kodi 50 zilizokuwa zikiwakwaza wafanyabiashara lengo likiwa ni kuwawezesha kufanyabishara yao kwa ufanisi zaidi ili waendelee kulipa kodi

“Tumepunguza kodi nyingi sana!, Mwaka uliopita wa fedha (2018/2019) tulipunguza kodi 108 na mwaka huu wa fedha (2019/2020 tumepunguza kodi na tozo 54 kwa makusudi, Dkt, John Pombe Magufuli ameamua kuwawezesha watanzania, kila mmoja kwenye eneo lake la kazi afyanye kazi vizuri” alisisitiza

Aidha, Dkt. Kijaji aliwataka wafanyabiashara waliopata msamaha wa riba kwenye kodi mbalimbali walizokuwa wanadaiwa, walipe madeni yao kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa na kwamba hakutakuwa na muda mwingine utakao ongezwa.

Aliwataarifu wafanyabiashara hao kwamba Serikali imesitisha kwa muda utoaji fedha kwenye miradi mikubwa ya kimkakati iliyopangwa kutekelezwa na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI yenye lengo la kuziwezesha Halmashauri kujitegemea kimapato hadi pale mfumo madhubuti wa kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo utakapo wekwa.

Dkt. Kijaji alitoa kauli hiyo baada ya kupokea maombi kutoka kwa Mbunge wa Babati Mjini Mhe. Pauline Gekul, aliyeomba shilingi bilioni 5.5 kutoka Serikalini kwa ajili ya kujenga kituo cha mabasi ili kuboresha mazingira ya biashara na utoaji huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake Naibu Kamishna Operesheni ya Kodi Bw. Simon Kingu, alisema TRA iko tayari kushirikiana na wafanyabishara na kuhakikisha wanatatua kero zao ili walipekodi kwa hiari kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Alisema juhudi kubwa inayofanywa na Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ya kuifikisha nchi katika uchumi wa kati wa viwanda unategemea mchango mkubwa wa wafanyabiashara katika kulipa kodi stahiki.

No comments:

Post a comment