Ferdinand Shayo,Arusha.
Shirika la Haki elimu limetoa kiasi cha shs 20 milioni kwa ajili ya kuchimba kisima cha maji katika shule ya sekondari Mukulat iliyopo katika halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru kilichogharimu shs 25 milioni .
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo ,Dokta John Kalage wakati akizungumza katika makabithiano ya kisima hicho kilichojengwa kwa ufadhili wa ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania.
Dokta Kalage alisema kuwa,ubalozi wa Uingereza umekuwa ukishirikiana na Haki elimu katika kuboresha mazingira ya elimu, na ufundishaji hasa kwa mtoto wa kike katika kuhakikisha idadi ya wanafunzi wanaojiunga katika shule hadi vyuo inaongezeka kwa asilimia kubwa.
Aliongeza kuwa, wamefikia hatua ya kusaidia shule hiyo baada ya kuwepo kwa changamoto ya wanafunzi wa kike kutembea umbali wa kilometa 8 kufuata huduma za maji.
Alisema kuwa, shirika hilo limekuwa likisaidia shule 127 ikiwemo shule hiyo na shule ya Ngiresi lengo likiwa ni kusaidia kuboresha mazingira ya mtoto wa kike ili waweze kuongeza kiwango cha idadi hiyo kuwa kubwa kuanzia elimu ya msingi hadi chuo.
" takwimu zinaonyesha kuwa ,watoto wa kike wamekuwa wakiandikishwa kwa wingi katika shule za msingi kuliko wa kiume lakini ukija kwa masomo ya elimu ya juu mwitikio wa wasichana ni mdogo sana,ambapo kwa kipindi cha miaka mitano hadi sita iliyopita inaonyesha asilimia 5 hadi 6 ya wasichana wamekuwa wakiendelea na kidato cha tano huku wavulana ikiwa ni asilimia 12 hadi 13."alisema Dokta Kalage.
Naye Mwalimu mkuu wa shule hiyo ,Vitalis Nada alisema kuwa,wamepata fursa ya kutembelewa na Balozi huyo kwa ajili ya kujionea mradi wa kisima cha maji kilichofadhiliwa na ubalozi ambapo kimeweza kuondoa changamoto kubwa ya wasichana wanaolala bwenini kutembea umbali mrefu.
Nada alisema kuwa, pamoja na kuwa shule hiyo inazungukwa na jamii ya wafugaji,wamekuwa wakijitahidi sana kuhakikisha kiwango cha elimu hasa kwa watoto wa kike kinakuwa juu kwa kuboresha mazingira shuleni hapo,ambapo imesaidia sana kiwango cha elimu kwa wasichana kuendelea kupanda kila mwaka.
Alitaja changamoto inayowakabili kuwa ni pamoja na changamoto ya uhaba wa mabweni kwa ajili ya wasichana ambapo wana mabweni mawili tu ambayo yanalaza wanafunzi 84 ,huku shule nzima ikiwa na wasichana 520, hivyo wanafunzi 436 wana uhitaji wa mabweni hayo.
Kwa upande wa Balozi wa Uingereza nchini Tanzania ,Sarah Cooke alisema kuwa, wamekuwa wakisaidia shule mbalimbali kuondokana na changamoto mbalimbali katika sekta ya elimu huku lengo kubwa likiwa ni kusaidia zaidi wasichana ili waweze kuwa na mwamko wa kupenda elimu zaidi.
Post A Comment: