Na Lucas Myovela_Arusha

SERIKALI  imesema kuwa itahakikisha inaendelea kushirikiana na wawekezaji hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuwawekea  mazingira mazuri ili waweze kufanya shughuli zao pasipo kuwa na bughudha  zozote kwani
wamekuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa pato la Taifa.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Mifugo,Elisante ole Gabriel aliyasema hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa katika ziara yake ya kutembelea kiwanda cha kusindika nyama cha Happy Sausage kilichopo
Sakina jijini Arusha.

“Wawekezaji wamekuwa na mchango mkubwa sana katika kuinua pato la taifa pamoja na uchumi wa nchi kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kuchangia kupatikana kwa ajira nyingi kwa wananchi hivyo hawana budi kuthaminiwa kwa mchango wao huo’’alisema Katibu Mkuu huyo.

Ole Gabriel alisema kuwa anatambua changamoto mbalimbali zinazokikabili kiwanda hicho cha Happy Sausage ikiwemo mgogoro wa muda mrefu kati yake na halimashauri ya jiji la Arusha hali ambyo imekuwa ikichangia kusuasua kwa uzalishaji wa bidhaa kiwandani hapo na kuhahidi kulipatia ufumbuzi ndani ya muda mchache.

Awali akimkaribisha Katibu Mkuu huyo,Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa kiwanda hicho,Andrew Mollel alimweleza katibu mkuu huyo kuwa kiwanda hicho kilianzishwa mwaka 1990 na kwamba kimekuwa kikizalisha bidhaa zenye ubora ambapo kwa sasa kimejipanga kutanua soko lao kufikia nchi zote za Afrika Mashariki.

“Kiwanda kimeshindwa kufikia malengo ya kuongeza uzalishaji kutokana na kujikuta kwamishwa kufanya ukarabati wa kiwanda hicho ilihali serikali kupitia vizara ya mifugo na uvuvi kwa nyakati tofauti imekuwa ikikitaka kiwanda hicho kufanya ukarabati imekuwa ndio changamoto yetu kufikia malengo ya uzalishaji”.alisema Mollel.

Mwenyekiti huyo wa bodi aliongeza kuwa pia halimashauri ya jiji la Arusha imekuwa ikikwamisha ukuaji wa kiwanda hicho kwani imekataa kutoa kibali cha ukarabati na upanuzi wa majengo ya kiwanda hicho (building permit) jambo linalokwamisha uongezaji wa thamani na uzalishaji hali ambayo imekuwa  ni changamoto kubwa sana kwao na kuiomba serikali kuu kuingilia kati swala hilo.

Mollel aliiomba Serikali iweze kuwapatia eneo lenye ukubwa wa ekari 300 katika eneo la Muriet jijini hapa ili aweze kuanzisha shamba kubwa la mifugo litakalokiwezesha kiwanda hicho kufuga mifugo mingi ikiwemo nguruwe kwani tayari  wamekwishafanya mazungumzo na serikali ya Ujerumani ambapo imewaahidi kuwapatia mbegu za nguruwe wanaokua kwa muda mfupi ukilinganisha na  wa hapa Tanzania ambao huchukua muda mrefu kukua.

Share To:

Lucas Myovela

Post A Comment: