Na Ado Shaibu.

Kabla ya kuandika chochote ninaona ni hekma kutangaza kwanza maslahi kuwa mimi ni Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano na Umma wa chama cha ACT Wazalendo.

 Nafasi hii inanipa madaraka ya kuwa msemaji wa kauli na misimamo rasmi ya chama.

Hata hivyo, yale nitayoyasema kwenye makala haya na nyingine zitazofuata kwenye safu hii zinahusiana na mitizamo na fikra zangu binafsi.

Hivyo basi, tafakuri hii isifungamanishwe na ACT Wazalendo.

Ukiacha maslahi yangu ya kichama, hata kabla ya kujiunga na siasa za vyama, nimekuwa mwanaharakati ninayeamini katika misingi ya utu, demokrasia, usawa na uzalendo.

Andiko hili na yale yatayofuatia katika safu hii ni katika kutekeleza wajibu wangu wa kuipigania na kuilinda misingi hiyo ninayoiamini.

Tuingie kwenye mada yetu ya leo. Ili tuweze kusafiri kwenye jahazi moja kifikra hatuna budi kurejea miaka miwili na ushei nyuma.

Mwaka 2017, ikiwa ni miezi michache tangu ateuliwe kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo alikaririwa na gazeti moja la Kiswahili (si gazeti hili) kuwa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, Rais Magufuli atachaguliwa kwa kishindo bila kuwa na upinzani.

Katika kunogesha hoja yake, Profesa Mkumbo alisema kwamba iwapo miradi ya maji iliyotekelezwa na iliyo mbioni kutekelezwa itafanikishwa, Rais Magufuli hatalazimika kupiga kampeni bali atakuwa anatembea na kupunga mkono tu kuanzia Dar es salaam hadi Kigoma!

Binafsi sikukubaliana na Mwalimu waangu Profesa Mkumbo. Hivyobasi, bila kupoteza muda nilifanya uchambuzi wa kumjibu ambao ulichapishwa na gazeti hili mwaka 2017.

Kwenye uchambuzi wangu niliweka wazi kuwa vigezo vitavyoamua ushindi wa uchaguzi wa mwaka 2020 ni haki na uchumi.

Kwa kuzingatia vigezo hivyo, nilijenga hitimisho kuwa kwenye uchaguzi wa huru na wa haki, Rais Magufuli si tu hawezi kushinda kwa kishindo bali kuna uwezekano mkubwa asishinde kabisa.

Hivi sasa, miaka miwili baada ya andiko langu la mwaka 2017, imani yangu bado ipo palepale. Kwa hakika, imani hiyo imeimarika maradufu kwa sababu, kwa maoni yangu, serikali ya awamu ya tano imeendelea kuyavuruga zaidi maeneo hayo mawili ambayo, kwa maoni yangu, ndiyo yataamua mshindi wa uchaguzi mkuu wa mwaaka 2020.

Kwa upande wa haki, serikali ya awamu ya tano imeweka rekodi ya kuwa kinara wa uvunjaji wa haki za raia kuliko utawala wowote ule tangu Tanganyika na Zanzibar zipate uhuru. Hivi sasa Watanzania wanaishi kwenye hofu kubwa kutokana na utawala wa mabavu.

Tanzania ya leo imekuwa Tanzania ya waandishi wa habari kuzibwa midomo na wale wenye msimamo kupotezwa, kubambikiwa kesi au kutishwa; wanaharakati kutekwa, kuteswa au kuuawa; vyama vya siasa vya upinzani kunyimwa nafasi ya kufanya siasa huku Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikifumbia macho; wafanyabiashara kubambikiwa kodi kubwa, kufilisiwa na kubambikiwa kesi; mabinti wanaopata ujauzito kunyimwa fursa ya kuendelea na masomo; viongozi wa dini (kama vile Mashehe wa Uamsho) kuozea rumande bila kesi ya msingi; wavuvi kufukarishwa na wengine kuuawa bila wanaofanya hivyo kuwajibishwa. Orodha ya madhila ni ndefu na hatuwezi kuimaliza hapa.

Jambo la msingi ni kuwa angalau kila kundi kwenye jamii limeonja adha ya utawala wa kimabavu wa serikali ya awamu ya tano. Wakulima, wafanyabiashara, wanafunzi, wafanyakazi, wavuvi, waandishi wa habari, wanasiasa, viongozi wa dini, Asasi za Kiraia na kila kundi kwenye jamii limeguswa.

Hakuna aliye salama, ndani na nje ya serikali, ndani na nje ya CCM, ndani na nje ya nchi! Kila mmoja ameguswa na rungu!

Kwenye uchumi vilevile mambo ni shelabela. Awamu ya tano imejipambanua kuwa ni yenye kuhusudu zaidi maendeleo ya vitu badala ya maendeleo ya watu. Vipaumbele vya serikali hivi sasa ni maeneo kama vile miradi ya nishati, reli na ndege ambayo kwa kweli kwa jinsi inavyoendeshwa, haina mafungamano ya moja kwa moja na kumkwamua Mtanzania kutoka katika lindi la umasikini.

Serikali ya awamu ya tano imezipa kisogo sekta za kilimo, uvuvi, afya, elimu na maji ambazo  zina mafungamano ya moja kwa moja na kumkwamua Mtanzania wa kawaida kutoka  katika dhiki.

Ukitazama mfano wa sekta ya kilimo peke yake, awamu hii imejipambanua kuwa kinara wa kuuwa mfumo wa uzalishaji na masoko wa mazao karibu yote makubwa ya biashara kama vile korosho, tumbaku, kahawa, mbaazi na hivi sasa pamba.

Ukiacha hadaa na propaganda zinazoenezwa na CCM na washirika wake kupitia vyombo vyao vya habari, ukweli ni kwamba mazingira ni mazuri zaidi hivi sasa kuiondosha CCM madarakani pengine kuliko kipindi kingine chochote kilichopita.

Lakini, jambo hili linahitaji vuguvugu kubwa la umma linalowaleta pamoja wadau na makundi yote yaliyokandamizwa na kuguswa na utawala huu. Kuyaunganisha makundi haya sio kazi nyepesi. Ni kazi inayohitaji, pamoja na mambo mengine, uongozi madhubuti.

Kwa maoni yangu, Zitto Kabwe (Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo) na Tundu Lissu (Aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA) wamejenga taswira ya kuwa vinara wa vuguvugu la upinzani dhidi ya serikali iliyopo madarakani.

Hivyobasi, wote wawili wana wajibu wa pamoja wa kuyaunganisha makundi mbalimbali yaliyoguswa na utawala wa sasa. Hii ni kazi ngumu inayohitaji hata kabla ya kuianza, kuvivuka vikwazo kadhaa ikiwemo vya kibinafsi, vya taasisi zao na mitego ya dola.

Kwa leo nitue kalamu yangu hapa. Pengine msomaji wangu utakuwa na maswali kadhaa kwangu; kwa nini Zitto na Lissu? Wajibu wao ni upi? vikwazo vyao ni vipi? Vipi kuhusu urais 2020, nani agombee? Maswali haya na mengine mengi nitayajibu wiki ijayo.

Simu: 0653619906

Baruapepe: adoado75@hotmail.com
Share To:

msumbanews

Post A Comment: