Tuesday, 3 September 2019

Afisa Tarafa Elerai Aagiza Mzazi Aliyewafanyia Vurugu Walimu Akamatwe


Na Ferdinand Shayo,Arusha.
Afisa Tarafa wa Elerai Elerai ,Titho Cholobi ameagiza Mzazi aliyefika  katika shule ya sekondari Olasiti na mwanae  akiwa na tatizo la utoro akamatwe na kufikishwa polisi kwa kuwafanyia vurugu  walimu wa shule hiyo na kutokomea kusikojulikana  ili iwe fundisho kwa wazazi wengine wanaowadhalilisha walimu licha ya matatizo ya utoro na utovu wa nidhamu ya watoto wao.
Cholobi memtaka Mkuu wa Shule hiyo Fulgence Moshiro  kukata RB na kumfikisha kituo cha polisi mzazi huyo kwani alipaswa kushirikiana na walimu kutatua changamoto za mwanae mtoro badala ya kuwa upande wa mtoto wake na kuwatukana walimu.
Afisa huyo amebaini hayo baada ya kufanya ziara ya kukagua ujenzi wa jengo la utawala katika shule hiyo pamoja na kupata taarifa za maendeleo na changamoto za shuleni hapo ambapo mkuu wa shule hiyo alitoa taarifa ya kukithiri kwa utoro shuleni hapo kutokana na kukosekana kwa uzio.
“Tunashukuru sana serikali imetujengea jengo la utawala ambalo limekaribia kukamilika changamoto tuliyonayo kwa sasa ni upungufu wa matundu ya vyoo kwa wanafunzi pamoja na kukosekana kwa uzio ambako kunachangia utoro japo tunajitaidi kukabiliana nalo”  Alisema Mwalimu Mkuu
Hata hivyo mwalimu huyo aliwataka wazazi kushirikiana na walimu katika kutokomeza tatizo la utoro badala ya kushiriki kuwa upande wa wanafunzi na wakati mwingine wakiitwa shuleni na kuwatukana walimu na kuwadhalilisha jambo ambalo linawakatisha tamaa kama ilivyotokea shuleni hapo majira ya asubuhi.
Diwani wa kata ya Olasiti Alex Marti  amewataka viongozi kuendelea kushirikiana kwani tayari amepata wadau ambao wamejitolea kushiriki kujenga uzio kwa kushirikiana na mchango wa viongozi na wananchi.

No comments:

Post a Comment