Na WAMJW- MBEYA

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya inajenga jengo la Wazazi lenye thamani ya shilingi Bilioni 7 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ya kuboresha huduma za Afya kwa wananchi wa Mkoa wa Mbeya na nyanda za juu kusini.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za Afya na ujenzi wa miradi katika Hospitali ya Rufaa ya kanda Mbeya.

Waziri Ummy amesema kuwa Serikali imedhamiria kuboresha upatikanaji wa huduma za Afya nchini ikiwemo huduma za kibingwa ili kuondoa usumbufu kwa Wananchi wanaohitaji huduma hizo kwa kusafiri umbali mrefu i jambo linalopelekea gharama kubwa na usumbufu kwa wananchi.

"Tunajenga jengo la wazazi na watoto wachanga la ghorofa sita, ambalo litakuwa na jumla ya vitanda 200, vyumba vitatu vya upasuaji kwa ajili ya wanawake wajawazito ,vyumba sita kwa ajili ya uangalizi maalum (ICU) kwa wanawake wajawazito, pia vyumba maalum vinne kwa ajili ya vitoto vichanga (NICU)" alisema Waziri Ummy.

Kwa upande mwingine, Waziri Ummy amemwagiza Mkandarasi wa majengo hayo kuhakikisha wanaharakisha ujenzi wa majengo hayo ili wananchi waanze kupata huduma mapema jambo litalosaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto nchini.

Aidha, Waziri Ummy ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Mbeya na nyanda za juu kusini kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya ili kurahisisha gharama za matibabu.

"Nitoe Wito kwa wananchi wa Mkoa wa Mbeya na nyanda za juu kusini ili waweze kufurahia huduma nzuri lazima wajiunge na huduma za Bima ya Afya, Kuna NHIF Toto Afya kadi kwa mtu yoyote mwenye umri wa chini ya miaka 18 ni shilingi 50,400 huduma mwaka mzima ndani ya Mbeya na Tanzania kwa ujumla" alisema Mhe. Ummy Mwalimu

Kwa upande mwingine, Waziri Ummy amesema kuwa katika kila wanawake 100, wanawake 85 wanajifungua bila matatizo yoyote, huku akisisitiza kukamilika kwa ujenzi huu kutasaidia kukokoa wanawake 15 waliobaki kutokana na huduma Bora zakibingwa zitakuwa zikitolewa.

Naye, Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya kanda Mbeya Dkt. Godlove Mbwanji ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kukubali kutenga fedha ili kujenga jengo la ghorofa sita katika kitengo cha wazazi Meta ambalo litakuwa na uwezo wa vitanda 200 jambo litalosaidia kutatua changamoto ya ufinyu wa nafasi.

"Tunapenda kutoa shukurani za dhati kwa Serikali ya awamu ya tano, kwa kukubali kutenga fedha kupitia Wizara unayoiongoza ili kuweza kujenga jengo la ghorofa sita katika kitengo cha wazazi Meta, ambalo litakuwa na uwezo wa vitanda 200." Alisema Waziri Ummy

Mwisho.




Share To:

Post A Comment: