Wednesday, 8 May 2019

Kamati ya PAC yampa siku 7 Bosi wa TPA


Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imetoa siku saba kwa Mtendaji Mkuu wa Bandari (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko Kuhakikisha anafika mbele ya kamati hiyo Mei 14, mwaka huu na si vinginevyo.

Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Naghenjwa Kaboyoka wakati wa kikao cha kamati baada ya mkurugenzi huyo kushindwa kufika katika kikao hicho jambo ambalo kamati imeliona kuwa ni kulizarau Bunge zima.

Kwa mujibu wa Kaboyoka, kamati imeshindwa kufanya kazi yake ipasavyo kutokana na mtendaji huyo kushindwa kufika mbele ya kamati hiyo bila kutoa taarifa huku akisisitiza kuwa endapo kiongozi huyo hatotii agizo hilo hatua kali za kisheria zitachulkuliwa dhidi yake.

Awali Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dkt Leonard Chamuriho alikiri kutokutokea kwa mtendaji mkuu huyo wa TPA huku akibainisha kuwa ameshindwa kufika kutokana na matatizo ya kiafya na kuongeza kuwa licha ya kutokuweza kufika kwa mtendaji mkuu huyo waliamini wao wangeweza kuwakilisha vema katika kikao hicho na hivyo kuomba radhi kwa kamati hiyo.

Kwa kauli moja wabunge hao ambao pia ni wajumbe wa kamati ya PAC wamelaani kitendo hicho walichodai ni cha dharau kiliyoonyeshwa na mtendaji mkuu huyo wa TPA.

No comments:

Post a comment