Waziri wa Habari , Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amewataka watumishi wa wizara hiyo  kutimiza wajibu wao katika kutekeleza majukumu ya kila siku ili kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kutatua kero na kujibu hoja za wananchi kwa ufanisi na haraka.

Hayo ameyasema leo Jijini Dodoma alipokuwa akifungua Baraza Jipya la Wafanyakazi wa wizara hiyo  ambalo hukutana mara mbili kwa mwaka kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali yanayohusu utendaji na maslahi ya  watumishi.

“Napenda kusisitiza kuwa vikao  vya baraza la wafanyakazi vitumike kujadili malengo na mipango ya wizara ikiwa ni pamoja na maslahi ya watumishi ” Dkt. Harrison Mwakyembe

Ameongeza kuwa mabaraza ya wafanyakazi yapo kwa ajili ya kujadili utendaji wa kila siku  na jinsi ya kuboresha zaidi utendaji huo unaolenga kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi.

Aidha Dkt. Mwakyembe amewaagiza Wakuu wa Idara na Vitengo  kusimamia kwa dhati suala la maadili katika sehemu za kazi kwa kuhakikisha watumishi wanatumia muda wa kazi vizuri kuwahudumia wananchi.

Kwa Upande wa Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo  Bibi. Susan Mlawi amewakumbusha watumishi kushiriki kikamilifu na kuwa mstari wa mbele katika kupambana na VVU/UKIMWI.

“Ugonjwa wa UKIMWI unagharimu Taifa  hivyo nasisitiza kuwa kiini cha ufanisi katika vita hii ni kwa kila mmoja wetu kubadili tabia” Katibu Mkuu Bibi. Susan Mlawi.

Pia amewasisitiza watumishi hao kufanya kazi kwa weledi ,bidii na tija kwa kuwa hakuna haki bila wajibu.

Naye Mwenyekiti wa TUGHE Tawi Bibi Magreth Mtaki amesema kuwa Baraza la Wafanyakazi linasaidia wafanyakazi kujadili na kuboresha utendaji kazi wa Wizara ili kuleta maendeleo ya Taifa.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: