Tuesday, 9 April 2019

Shilingi Milioni 478 Zatumika kujenga kituo cha Afya cha Manyire ArumeruSerikali ya Japani kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania imezindua kituo cha afya kijiji cha Manyire kata ya Mlangarini wilayani Arumeru mkoani Arusha kilichogharimu zaidi ya kiasi cha shilingi milioni 478 Fedha za kitanzania.

Akiongea na Balozi wa Japan ofisini kwake muda mfupi kabla ya uzinduzi wa kituo hicho Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Jerry Muro ameuomba ubalozi huo kuwasaidia katika upatikanaji wa mitaji kwa makundi ya vijana hususani katika sekta ya kilimo na ufugaji wilayani humo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha Dkt. Wilson Mahera amesema kituo hicho hadi kukamilika kimetumia Milioni 478, ambapo miongoni mwa pesa hizo kiasi cha milioni 191 zilitolewa na serikali ya Japan na milioni 120 ilitolewa na aliyekuwa diwani wa kata hiyo ambaye kwa sasa ni mstaafu Mathias Manga pamoja na nguvu za wananchi ambao wamechangia milioni 20.

Aidha amesema kuwa Halmashauri ilitoa zaidi ya milioni 80 kwa ajili ya kumlipa mkandarasi pamoja na kununua vifaa mbalimbali ikiwemo vitanda na kuleta wahudumu wa afya katika kituo hicho.

Naye Balozi wa Japan, Shinichi Goto ameshukuru kwa ukamilikaji wa kituo hicho na kuahidi kuwa serikali hiyo itaendelea kuchangia maendeleo katika nchi ya Tanzania kwa kadri watakavyofanikiwa ambapo amesema wako tayari kwa ajili ya kutafuta fedha za kuwasaidia vijana mitaji katika sekta ya kilimo na ufugaji kama alivyoeleza Mkuu wa Wilaya hiyo.

Hata hivyo Balozi huyo amesema serikali ya Japani imewekeza molioni 195 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari Sokoni 2 iliyopo wilayani Arumeru mkoani Arusha. Kama njia moja wapo ya kuunga mkono jitihada za serikali ya Tanzania katika maendeleo ya sekita ya Elimu .

No comments:

Post a comment