Na. Mwandishi Wetu

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Stella Ikupa amelipongeza Shirika lisilo la kiserikali la Compassion International Tanzania (CIT) kwa kuwahudumia na kuwapatia watoto na vijana stadi za maisha zinazowawezesha kujitegemea.
Stella ametoa pongezi hizo wakati wa Maadhimisho ya Miaka 20 ya Shirika hilo yaliyofanyika leo Aprili 27, 2019 katika ukumbi wa Kanisa la TAG lililopo Mipango, Jijini Dodoma.

Maadhimisho hayo yalikuwa na Kauli Mbiu isemayo; “Wekeza kwa Watoto na Vijana kwa Uchumi Endelevu.”

Ameeleza kuwa Shirika la Compassion International Tanzania limekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha watoto na vijana nchini wanahudumiwa na kuondokana na hali ya umasikini kwa kuwa chachu ya maendeleo kwa jamii na Taifa.

“Shirika hili ni la mfano na limeendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuwalinda watoto na kuwapa fursa ya kufikia ndoto zao na kuwapatia vijana ujuzi wa stadi za maisha zinazoleta mabadiliko chanya kwao na kuwaletea maendeleo yao binafsi na Taifa kwa ujumla,” amesema Stella

Ameongeza kuwa Rais Dkt. John Magufuli amekuwa akionesha watanzania namna gani nchi yetu imeweza kujitegemea katika kutekeleza shughuli mbalimbali, hivyo Rais ni mfano tosha wa kuigwa na vijana nchini kwa kuona wanauwezo wa kujitegemea.

Aidha, Stella alitoa rai kwa vijana kuacha kukaa kwenye vijiwe bila sababu za msingi na kubadili mitazamo, bali watumie muda wao kutafakari shughuli za kufanya kwa bidii ambazo zitawaletea maendeleo na kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.

“Serikali imekuwa ikitoa mikopo kwa vijana ili waweze kuanzisha shughuli mbalimbali zitakazo wawezesha kukua kiuchumi, tumieni fursa ya ujuzi mliopata kupitia shirika hili na ubunifu mlionao kuchangamkia fursa hiyo muhimu itakayowawezesha kuanzisha miradi mbalimbali ikiwemo viwanda,” amesema Stella.

Pia alitoa wito kwa jamii kuripoti haraka vitendo vya unyanyasaji wa watoto katika madawati ya jinsia na watoto yaliyopo kwenye vituo vya polisi nchini na kwa maafisa ustawi wa jamii ili kutokomeza vitendo hivyo kwa kumjengea mazingira salama mtoto na kumuonesha jamii yake imejaa upendo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taifa wa Shirika la Compassion International Tanzania, Agness Hotay alisema kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha wanawatetea na kuwasimamia watoto na kuwapatia nafasi vijana ya kujitambua kwa kuchangamkia fursa ambazo zipo katika jamii na kuleta ufumbuzi wa kimaendeleo.   

“Maono ya shirika ni kuona wanufaika wanatoka katika uhitaji na kujijengea dhana ya kujitegemea, vilevile kuwa wahisani wa watu wengine,” amesema Hotay
Shirika la Compassion International Tanzania (CIT) ni sehemu ya Compassion International ambalo ni shirika la kimataifa la Kikristo linalojihusisha kuhudumia watoto na vijana wanaotoka katika kaya maskini kwa njia ya ufadhili.

Shirika hili limekuwa likifanya huduma hii hapa nchini toka mwaka 1999.

Kwa sasa Shirika hilo lipo katika Mikoa 19 ya Tanzania Bara ambayo ni Arusha, Dar es Salaam, Kigoma, Manyara, Pwani, Morogoro, Iringa, Dodoma, Kilimanjaro, Singida, Shinyanga, Mwanza, Mara, Tabora, Lindi, Geita, Mtwara, Simiyu na Kagera.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: