Sunday, 12 August 2018

Polisi - acheni kukabidhiana silaha za moto kienyeji


Jeshi la Polisi mkoani Arusha limetoa angalizo kwa baadhi ya Makampuni ya Ulinzi kuwa makini na silaha za moto na kuacha mara moja tabia ya askari wake kukabidhiana kwa kupeana kienyeji badala yake wafuate utaratibu.

Agizo hilo limetolewa leo na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng’anzi wakati akiongea na wawakilishi wa Makampuni ya Ulinzi mkoani hapa katika kikao kujadili mafanikio na changamoto za Makampuni hayo kilichofanyika ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi uliopo jijini hapa.

Kamanda Ng’anzi alisema baadhi ya askari wa Makampuni hayo wanapomaliza muda wa kuondoka lindoni wanakuwa na tabia ya kumkabidhi silaha askari anayeingia bila kuandikishana kwenye kitabu cha makabidhiano kitu ambacho si sahihi.

“Silaha ni Sensitive sana sio Muwa au Kanga unatakiwa utembee nayo wakati wote na hauwezi kuiacha popote au kukabidhi kienyeji kwani inapokwenda kwenye mikono ya watu hatari inaweza ikatumika vibaya na kuleta madhara makubwa, makabidhiano ya silaha yana taratibu zake”. Alilisitiza Kamanda Ng’anzi.

Alisema kwamba hali hii inaonyesha kwamba baadhi ya askari  wa Makampuni hayo wanahitaji mafunzo zaidi ili waweze kutambua umuhimu wa silaha na kuwaahidi kuwapatia wakufunzi watakaowapa mafunzo ya kutambua majukumu yao pamoja na haki zao.


Kamanda Ng’anzi alisema pamoja na changamoto kadhaa zilizopo ndani ya utendaji wa Kampuni hizo lakini zimekuwa msaada mkubwa katika masuala ya Usalama kwani mara nyingi wamekuwa wakifanya doria lakini pia kulinda katika maeneo mbalimbali.

Alisema Jeshi la Polisi mkoani hapa mara kwa mara limekuwa likishirikiana na Kampuni hizo kwa kupokea taarifa za uhalifu lakini pia kushirikiana nao katika kuimarisha ulinzi wakati wa Sikukuu kama vile Krismas na Mwaka Mpya ambapo Kampuni hizo zinajitolea kutoa Magari pamoja na askari wao.

Alizitaka kampuni ambazo zinamilikiwa na wazawa kuiga mifano ya Kampuni za nje ambazo zimewekeza nchini kwa kuzidi kuboresha viwango vya ubora, kuwa na vifaa bora na wabobezi katika sekta hiyo ili nazo siku moja ziweze kupata soko nje ya mipaka ya nchi yetu.

Akitoa historia fupi ya Makampuni ya Ulinzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Sekta Binafsi ya Ulinzi nchini Bw. Isaya Maiseli alisema kwamba, Sekta binafsi ya ulinzi nchini mwetu imeanza toka mwaka 1988 mara tu baada ya ubinafishaji wa njia kuu za uchumi .

Alisema awali maeneo mengi ambayo sasa baadhi yao yanalindwa na Makampuni ya Ulinzi yalikuwa yanalindwa na Jeshi la Polisi na Polisi Wasaidizi na kubainisha kwamba, Kampuni ya kwanza kabisa kuanzishwa ilikuwa inaitwa Simba Security na baadae kufuatia Kampuni nyingine ambapo mpaka hivi sasa kuna jumla ya Makapuni 759 huku mkoa wa Arusha ukiwa na Makampuni ya Ulinzi 53.

Awali akimkaribisha Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kikao hicho, Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii mkoani hapa Mrakibu Msaidizi (ASP) Edith Makweli alisema kwamba Makampuni hayo ya Ulinzi ni wadau muhimu sana kwa Jeshi la Polisi.

Alisema mara nyingi wamekuwa wakishirikiana nao katika masuala ya kiusalama na wao wana mchango mkubwa  katika kuimarisha utulivu wa mkoa huu, hivyo basi wataendelea kushirikiana nao na kuhakikisha Arusha inaendelea kuwa salama.

Jumla ya washiriki wapatao 40 walihudhuria katika kikao hicho ambapo mbali na Jeshi la Polisi mkoani hapa kuongelea mafanikio na changamoto za Makampuni hayo ya ulinzi lakini pia wawakilishi hao kwa mara ya kwanza walifanya uchaguzi na kufanikiwa kupata viongozi wao wa Chama hicho ngazi ya mkoa.

No comments:

Post a comment