Leo ninawaletea ufafanunuzi wa mambo yanayoashiria ufanano wa kiutendaji kati ya Mwl Nyerere na Ndg Magufuli Mwkt wa CCM na Rais wa Tanzania, kwa kuwa viongozi hufananishwa na hutofautishwa kwa utendaji wao katika kutoa uongozi.

-Ukweli

Mwalimu mwanzoni mwa miaka ya 1960 alipojiuzulu Uwaziri Mkuu kwenda kujenga Chama nakumuachia Serikali Mzee Kawawa, aliandika vitabu vitatu kimojawapo ni TUJIJISAHIHISHE ni kitabu kidogo chenye kurasa zisizozidi  ishirini ambapo amesisitiza katika kusema kweli na neno Kweli limetajwa zaidi ya mara ishirini.
"Ukweli unatabia moja nzuri sana, haujali mkubwa wala mdogo, haujali adui wala rafiki. Kwake watu wote ni sawa. Pia ukweli unayo tabia ya kujilipiza  kisasi kama ukipuuzwa.."

Hayo ni baadhi ya maneno katika kitabu hicho, yanayosisitiza kusema ukweli na kuheshimu ukweli. Hii ni sawa kabisa kwa Magufuli ambaye toka awali amekuwa ni kiongozi anayesisitiza kusema ukweli na kwa sasa ni mwasisi wa msemo "Msema kweli ni mpenzi wa Mungu".

-Kusimamia Misingi

CCM ina msingi wa vitu viwili, Haki na Watu. Mwalimu mwaka 1968, akitoa hotuba aliyoiita, "Lazima Chama Kiwasemee watu" na moja ya kauli zake ni, "kazi ya Chama cha Siasa kilicho imara ni lazima kiwe kama daraja la kuwaunganiaha watu na serikali walioichagua." Mwalimu alisema akiwaasa viongozi wa Chama kuwa karibu na wananchi na kuwa  watetezi wa haki za wanyonge.

Hiyo tunaishuhudia tena kwa Magufuli ambapo kwa kiasi kikubwa amekuwa  akiwasisitiza viongozi wa Chama kuwa sikio la wananchi na hata mageuzi ya Chama yamelenga kukifanya kuwa "Chama Cha wanachama na kinachoshughulika na shida za watu"

-Falsafa ya kazi

Mwaka 1976 Mwalimu aliandika kitabu "kila mtu afanye kazi" kinachoeleza kwa undani umuhimu wa kazi katika maisha binafsi na kwa taifa. Sasa ni miaka 40 Magufuli amekuja na falsafa inayofanana ya "Hapa Kazi Tu".

- Sera ya Viwanda na Kilimo

Mwalimu aliweza kuanzisha programu za kilimo ikiwemo "utekelezaji wa siasa ni kilimo" - 1974, sera ya viwanda vidogo vidogo (SIDO), vya kati ikiwemo viwanda vya nguo urafiki, Mwatex, Mutex, Mbeyatex, n.k Sawa kabisa na Magufuli ambaye ndoto yake ni Viwanda. Miezi miwili iliyopita amezindua mradi mkubwa wa kilimo awamu II utakaogusa maisha ya wakulima wadogo kwa kuwapatia mikopo nafuu ya kilimo.

-Udhibiti wa madini

Katika suala la madini Mwalimu alifanya utambuzi wa maeneo yenye madini, hakuruhusu uchimbaji uanze mbali na changamoto tulizokuwa tukizipitia kama Taifa, kwa kuwa Watanzania hatukuwa na elimu ya kutosha ya Madini. Magufuli amekuja amekuta mikataba kandamizi iliyoingiwa na watangulizi wake baada ya mwalimu hivyo ameifumua mikataba yote ya Madini na kufanya haki ya mtanzania kuheshimiwa na kuweza kuingia makubaliano kutoka 3% ya awali mpaka 50/50%.

- Reli, Umeme na Anga.

Mwalimu aliweza kujenga Reli ya TAZARA miaka ya 1970, kwa upande mwingine alikuwa na ndoto kubwa ya ujenzi wa mradi mkubwa wa umeme maarufu kama Stiegler's Gorge ambao ulikwamishwa, shirika la ndege lilikuwa na ndege za AirTanzania kabla halijafa katika awamu zilizofuata. Miaka 30 sasa Magufuli amefufua shirika la ndege na mpaka sasa serikali imefanikiwa kununua ndege Saba ndogo za kati na kubwa. Ujenzi wa Reli ya kisasa unaendelea naujenzi wa mradi mkubwa wa umeme wa Stiegler's Gorge umeanza.

Vijana wa miaka ya 1990, Nyerere tunayesimuliwa nakumsoma amerejea katika sura ya Magufuli na ni jukumu letu kumpa ushirikiano na kufanya naye kazi kuhakikisha tunatekeleza na kufikia ndoto ya TViwanda.

Na mwandishi wetu,
Said Said Nguya
Saidnguya@gmail.com
Share To:

msumbanews

Post A Comment: