Wednesday, 8 August 2018

CCM Monduli wagomea Kalanga kupitishwa bila kupingwa


Ikiwa ni siku chache baada ya aliyekuwa Mbunge wa Monduli kupitia CHADEMA , Julius Kalanga kujiuzulu na kuhamia CCM wanachama wa CCM, wilaya ya Monduli wameandamana kwenye ofisi za chama hicho wakitaka Kalanga kufuata utaratibu ikiwemo hatua za uteuzi wa nafasi ya kugombania ubunge.

Wakizungumza na wanahabari katika ofisi hizo wamesema wamesikia taarifa za kuteuliwa kwake bila kufuata utaratibu ikiwemo kukaa vikao na wazee wa kimila Malaigwanani ili waweze kumpitisha kugombea tena nafasi hiyo.

Wanachama hao wakiongozwa na baadhi ya wenyeviti wa matawi ya CCM wilayani Monduli wamesema chama kinaongozwa na katiba na hawatosita kupingana nao wakisisitiza taratibu zifuatwe.

“Tunamkubali mwenzetu aliyetoka upinzani hatukatai, lakini tunachokitaka sisi ni sheria zifuatwe aje azungumze na wananchi, aseme kuwa alishindwa kufanya nini akiwa nje ya chama na ameingia kwenye chama atatufanyia nini, bila kufanya hivyo sisi hatutashirikiana naye”, amesema mmoja ya waandamanaji.

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Monduli, Wilson Lengima amesema kuwa hajashiriki kwenye vikao na wazee wa kimila kama inavyodaiwa na baadhi ya wanachama hao na kwamba utaratibu utatumika katika kuwapata wagombea, na utawekwa wazi na mpaka sasa hakuna mgombea yeyote aliyepitishwa.

Usiku wa Julai 30, 2018 aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Monduli kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Julius Kalanga alijiuzulu na kujiunga na CCM kwa kile alichoeleza kuwa ni kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli na kudai kuwa ameondoka CHADEMA kwasababu ya siasa za chuki na uhasama.

No comments:

Post a comment