Wednesday, 18 July 2018

TRA yabaini wafanyabiashara 500 ya Utalii hawalipi kodi

Na Ferdinand Shayo, Arusha.
Mamlaka ya Kukusanya mapato Tanzania (TRA) imebaini wafanyabiashara wa utalii WA kujitegemea 500 maarufu kama freelance wasiokuwepo kwenye mfumo wa ulipaji kodi hivyo kusababishia serikali kupoteza mapato hivyo wameagiza wafanyabiashara hao kuwasilisha mikataba yao ili kuziba mianya ya upotevu wa mapato.

 (TRA) imefanya operesheni ya kukagua ulipaji wa kodi kwa watu wanaofanya biashara ya utalii na kuwaingiza watalii kupitia geti la Mamlaka ya Ngorongoro ikiongozwa na Kamishna wa kodi za ndani TRA,Elija Mwandumbya.

Kamishna huyo amesema kuwa wafanyabiashara wa utalii wanapaswa kuwasilisha mikataba yao ya kazi ili serikali iweze kupata stahiki na kuzuia udanganyifu.

Elija alisema kuwa serikali imejipanga kuhakikisha kuwa sekta ya utalii inakua na mchango mkubwa katika taifa ili serikali ipate fedha za kuendesha miradi ya maendeleo.


Mkaguzi wa zoezi hilo Emmanuel Marcel amesema kuwa wafanyabiashara wanaojitegemea wasiokua na idadi kubwa ya magari mengi wamekua wakitumia mwanya huo kukwepa kodi kuyaingiza magari yao kwenye kampuni zilizosajiliwa jambo ambalo wanalishughulikia kuhakikisha wanalipa kodi.

Kwa upande wao waongoza watalii Paul Kasmir wamesema kuwa kuwepo kwa mikataba itakayowasilishwa TRA itasaidia serikali kupata mapato pamoja na kulinda maslahi ya waongoza watalii.

Alisema kuwa zoezi hilo limefanyika bila kusababisha usumbufu kwa watalii jambo ambalo linapaswa kuigwa na taasisi nyingine.

Tanzania inakadiriwa kuwa na wafanyabiashara ya utalii 2200 ,Wafanyabiashara walioko kanda ya kaskazini ni 1403 huku Wafanyabiashara wanaojitegemea wasiotambulika ni zaidi ya 500 katika siku 20 tulizofanya ukaguzi.

No comments:

Post a comment