Na Atley Kuni- OR TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Said Jafo (Mb) ametoa siku mia moja na ishirini na tatu (123) kuanzia leo (tarehe 10 Julai, 2018) kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote zilizo pokea fedha za awamu ya tatu ya ukarabati wa vituo vya afya ziwe zimekalisha ujenzi huo.

Mhe. Waziri Jafo ametoa kauli hiyo akiwa mkoani Singida wakati wa ziara yake ya kukagua Vituo vya afya vinavyo endelea kujengwa nchi nzima.

Katika ziara hiyo, mkoani Singida  Mhe. Jafo amekagua kituo cha Afya Kintinku kilichopata fedha katika awamu ya kwanza milioni. 500  na kuridhishwa na hali ya ujenzi akiwa ziarani alipata pia wasaa wa kukagua eneo la ujenzi wa kituo cha Afya cha Nkonko kilichopokea Mil. 400 ambacho kitakarabatiwa na kuongezewa majengo manne. 

Mhe. Jafo alisema, fedha hizo zitatumika kukarabati jengo la mama na Mtoto, Jengo la upasuaji, Maabara sambamba na nyumba ya Mtumishi katika Kijiji hicho.

“Mil. 400 mlizopokea hapa kituo cha afya Nkonko, nataka ifikiapo Oktoba 30, 2018 ziwe zimefanya kazi nzuri kuzidi ile ya Kintinku” alisisitiza Waziri Jafo na kuongeza kwamba, zoezi hilo sio kwa Nkonko peke yake bali Halmashauri zote zilizo pokea fedha za awamu ya  tatu inayo husisha vituo vya afya 98.

Mhe. Jafo, Waziri mwenye dhamana na OR TAMISEMI, akitoa salaam za Mhe. Rais, alisema nia ya Serikali ya awamu ya tano ni pamoja na kumkomboa Mwananchi hususani kwa kumsogezea huduma bora za kijamii jirani.

“Ndugu zangu kabla yakuendelea na hutuba yangu, naomba nilete salaam za Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Mhe. Rais anasema anawapenda sana na anawashukuru kwa kumuamini na kumpa dhamana ya kuongoza Nchi yetu, yeye amesema atawalipa fadhila kwa kuwatumikia kwa nguvu zake zote na kuhakikisha huduma za jamii zinakuwa bora ikiwepo suala la afya.” Alisema Waziri Jafo na kuongeza kwamba, wananchi waendelee kumuombea ili kazi waliyompatia kwa miaka yake ya uongozi yeye na wasaidizi wake waweze kuikamilisha” alinukuliwa Waziri Jafo.

Mbali na kutoa salaam za Mhe, Rais Mhe. Waziri Jafo hakusita kuelezea jinsi Mbunge wa  Jimbo hilo la Manyoni Mashariki Mhe. Daniel Mtuka, anavyo pigania maendeleo ya jimbo lake,  Mhe. Waziri Jafo amewaambia wananchi wa Jimbo la Manyoni Mashariki kwamba siku zote Mbunge wao amekuwa akikumbushia suala la ukarabati wa kituo cha Nkonko na Kintunku vilivyopo katika Jimbo lake.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe. Miraji Mtaturu ambaye pia anakaimu nafasi ya Ukuu wa Wilaya ya Manyoni, aliye Mwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida katika ziara hiyo, alimuhakikishia Mhe. Waziri wa Nchi juu ya usimamizi madhubuti wa fedha hizo na kwamba hata kuwa na mzaha na yeyote atakayejaribu kwenda  kinyume na makusudio ya fedha hizo.

“Mhe. Waziri mimi nikuhakikishie kwamba, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa kuwa, kila shilingi itakayotumika katika ukarabati wa majengo ambayo imeletwa kwa ajili ya kituo hiki itafanya kama ilivyo kusudiwa na kwa mtu atakayethubutu kwenda tofauti hatutakuwa na huruma naye lazima mkondo wa sheria uchukue nafasi yake” alisema Mtaturu.

Awali akizungumza katika hafla hiyo Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki Mhe. Daniel Mtuka, alisema wananchi hao wapo tayari kufanya kazi kwa nguvu zao zote ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa ubora na kuzingatia thamani halisi ya fedha iliyotolewa.

“Nadhani Mhe. Waziri umekiona tulicho kifanya katika kituo cha afya Kintinku, sasa kwa moto ule ule chini ya Mkuu wetu wa Wilaya kijana wetu Mhe. Mtaturu anaye Kaimu kwa sasa nafasi ya Ukuu wa Wilaya, ambaye kwa kweli kama alivyo sema mwenyewe, mtu atakayejaribu kukwamisha shughuli za mradi huu atakwenda jela na hata muonea haya mtu wa aina hiyo”.

Mtuka alisema Mtaturu alisimama kidete Kintunku na wanaimani atasimamia vema na kutoa maelekezo sahihi katika kituo hicho cha Nkonko

Awali akiwa katika kituo cha Afya Kintinku, Waziri Jafo hakuacha kuwapongeza wananchi wa eneo hilo kwa kusema miongoni mwa Wilaya zilizofanya vizuri katika ukarabati wa vituo vya afya nchini ni pamoja na Kintinku.

“Leo Mhe. Rais anashuhudia katika vyombo vya habari, miongoni mwa watu mliofanya vizuri, watu wa Kintinku mmefanya vizuri sana sina budi kuwapongeza uongozi na wananchi kwa jumla jinsi mlivyo jitoa.” alisema Mhe. Jafo.

Wakizungumza kando ya mkutano huo wanachi katika maeneo ya Vijiji vya Kintunku na Nkonko wamepongeza jitihada zinazo chukuliwa na Serikali ya awamu ya tano ya kuwaboreshea huduma za afya.

Serikali katika awamu ya tatu ya ukarabati wa vituo vya afya, imetoa jumla ya fedha za kitanzania Shilingi Bilioni 38.9 ambazo zimeelekezwa kwenye ujenzi wa vituo vya  afya vipatavyo 98 kote nchini.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: