Thursday, 12 July 2018

Serikali Kufuta Tozo Ya Usajili,kuhuwisha Na Kushikilia Usajili Kwa Wawekezaji Wa Ndani

NA WAMJW-MWANZA
SERIKALI kupitia wizara ya afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto imefuta tozo ya usajili , kuhuwisha pamoja na kushikilia usajili wa bidhaa zao kwa wawekezaji wa ndani kupitia Mamlaka ya chakula na Dawa TFDA .

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati alipotembelea kuangalia ujenzi wa jengo la TFDA ambalo linajengwsa Jijini Mwanza ili kusogeza huduma kwa wananchi wa mkoa huo.

“Ili kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. John Pombe Magufuli za kukuza nchi kupitia uchumi wa viwanda hivyo TFDA msiwe kikwazo kwa wawekezaji hao hivyo kuanzia leo nafuta tozo za kusajili bidhaa,kuhuwisha bidhaa na tozo ya kushikilia usajili wa bidhaa”, alisema Waziri Ummy.

Aidha Waziri Ummy amesema kuwa kuendana na juhudi hizo pia Serikali  imefuta tozo ya udhibiti ya thamani ya 0.25 za dawa,vifaa na vifaa tiba zinazoingizwa kwenye hospitali za Umma kutoka kwa wafadhili.

Mbali na hayo Waziri Ummy amesema kuwa TFDA ina wajibu wa kusimamia Tanzania isiwe jalala la bidhaa zisizo na ubora kwa watanzania hivyo wanatakiwa kuweka afya ya wananchi mbele kuliko manufaa binafsi.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TFDA Bi. Agness Kijo amesema kuwa ujenzi wa jengo hilo ukikamilika utasaidia kuhudumia huduma za kimaabara kwa bidhaa zinazoingia nchini kwani itakuwa sio lazima tena kwenda kupima bidhaa hizo jijini Dar es salaam.

“Maabara hizi zikikamilika zitasaidia kufanya vipimo na udhibiti wa bidhaa katika mipaka mingi ya kanda ya ziwa ikiwemo Silali,Lusumo na Mtukula ili kuweka usalama wa bidhaa zinazoingia na kutoka nje ya nchi kwa usalama wa wananchi.

Sambamba na hilo Waziri Ummy alipata nafasi ya kutembelea kukagua ujenzi wa jengo la wodi ya mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou toure na kuhakikisha ujenzi unakamilisha ili kuokoa vifo vya mama na mtoto vinavyotokana na uzazi.

“Kama watu wa mwanza wanaridhishwa na huduma zinazotolewa katika hospitali hii basi ni lazima huduma za afya ziboreshwe ikiwemo afya ya mama na mtoto hivyo ninaleta mashine ya CT Scan kwa ajili ya kuboresha matibabu hapa” alisema Waziri Ummy.

Aidha Waziri Ummy aliwataka watendaji wa Hospitali  kutoa taarifa za utendaji kwa Waziri wa Afya na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo pamoja na kusimamiwa na Wakuu wa Mikoa yao ili kuimarisha huduma za afya nchini.

No comments:

Post a comment