Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  amewashauri Wana Habari wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kuendelea kuwa wabunifu zaidi wa vipindi  vitakavyoleta mvuto na hatimae kuwa na  wasikilizaji wengi zaidi wa Shirika hilo Nchini.

Alisema licha ya kuwepo kwa vipindi vingi vilivyokuwa maarufu  na kukubalika kwa wasikiizaji wengi akitolea mfano Kipindi cha Mawio na Maelezo baada ya Habari lakini bado juhudi za ubunifu zinahitajika katika kuona Mfumo wa Matangazo unawafikia Wananchi wengi zaidi Mjini na Vijijini.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa ushauri huo wakati alipofanya ziara fupi katika Kituo cha Matangazo cha Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC – REDIO) kiliopo Rahaleo Mjini Zanzibar kuangalia shughuli za utendaji kazi wa Taasisi hiyo ya Habari na kuridhika na jitihada zinazochukuliwa na Watendaji wawake.

Alisema upo umuhimu wa vipindi na matangazo ya ZBC Redio kuangaza zaidi kwa upande wa Majimboni na Vijijini ili Wananchi wa maeneo hayo wawe na fursa ya kuwasilisha changamoto zinazowakabili hasa katika harakazi zao za kujiletea maendeleo.

Balozi Seif alieleza kwamba wakati Serikali Kuu inafikiria jitihada za kusaidia changamoto zinazowakabili watendaji wa Kituo hicho cha Matangazo ya Radio ambapo pia kupitia nafasi yake ya Uwakilishi atajaribu kuwashawishi Wawakilishi wenzake majimboni kutoa ushirikiano utakaowezesha kuendelezwa kwa Vipindi vya kutoka Majimboni.

Alisema vipo vipindi vinavyoweza kusaidia Wananchi kuelimika zaidi ambavyo vinapaswa kupewa umuhimu wa pekee ili kupunguza kero zinazowakabili sambamba na kumrahisishia Mwakilishi kutekeleza majukumu yake badala ya kusubiri Vikao vya Baraza la Wawakilishi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: