Jeshi  la Polisi mkoani Dodoma limemkamata mfanyakazi wa kituo cha mafuta cha Afro Oil, kilichopo Ipogoro mkoani Iringa, Charles Mbise (23), akijaribu kutoroka baada ya kudaiwa kumuibia mwajiri wake Sh. milioni 17.9.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani humo, Gilles Muroto, mfanyakazi huyo alikamatwa juzi katika eneo la Mkonze jijini Dodoma majira ya saa 10.30 jioni, akiwa ndani ya gari namba T.165 DAD, aina ya Costa la kampuni ya Nani Kaona, akijaribu kutoroka kwenda mkoani Arusha.

Alisema Mbise alipora kiasi hicho juzi majira ya saa 3.30 asubuhi baada ya kumtishia kwa kisu meneja wa kituo hicho, Msimu Hassan.

Alieleza kuwa meneja huyo alilazimika kutoa fedha alizokuwa akizipeleka benki na kumpatia mtuhumiwa huyo na baada ya kufanya tukio hilo alimfungia ofisini.

Muroto alisema jeshi hilo baada ya kupata taarifa hizo walifanya msako kwenye magari yote yanayotokea Iringa.

"Tulifanikiwa kumkamata mtuhumiwa akiwa na fedha zote alizoziiba, kisu alichotumia kutishia na funguo za ofisi alizoondoka nazo baada ya kumfungia meneja ofisini. Tulimkamata majira ya saa 10. 30 jioni jana (juzi), akiwa ndani ya gari hilo katika eneo la Mkonze jijini Dodoma,” alisema Muroto.

Akizungumzia tukio hilo, mmoja ya wakurugenzi wa Kampuni ya Afro Oil, Salim Ahmed, alisema baada ya mfanyakazi wake kufanya tukio hilo, aliwasiliana na polisi mkoa wa Dodoma kwa sababu aliamini mtuhumiwa angekimbilia mkoani Arusha kupitia Dodoma.

“Tulitoa taarifa hizi polisi na pia zilisambaa picha za mtuhumiwa kwa polisi ambazo ziliwezesha kutambulika kwa urahisi,” alisema.

Alilipongeza jeshi hilo kwa namna lilivyofanikiwa kumnasa mtuhumiwa huyo kwa haraka akiwa na fedha taslimu alizoziiba huku akiahidi kampuni hiyo itajenga kituo kidogo cha polisi kwenye eneo lolote la Dodoma ambalo linachangamoto ya uwepo wa matukio ya kihalifu.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: